Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 07 14Article 546970

Habari za michezo of Wednesday, 14 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Polisi Tanzania yarejea baada ya ajali 

Polisi Tanzania yarejea baada ya ajali  Polisi Tanzania yarejea baada ya ajali 

TIMU ya Polisi Tanzania imeendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar kesho kwenye uwanja wa Ushirika.

Maafande hao wameanza mazoezi ikiwa ni siku chache zimepita tangu kupata ajali wakitokea mazoezini ambapo wachezaji kadhaa walijeruhiwa na mmoja Gerald Mdamu alivunjika miguu yote miwili.

Akizungumza jana, Ofisa habari wa timu ya Polisi Tanzania Hassan Juma alisema wachezaji saba kati ya wale waliopata ajali hawatacheza tena msimu huu mpaka watakapopata taarifa zaidi na daktari.

Alisema mazoezi yameanza ambapo wachezaji 12 wa kikosi hicho wameungana na wachezaji wa timu ya vijana watano ili kuongeza nguvu na kueleza wanashukuru waliojeruhiwa wanaendelea kupatiwa matibabu.

“Kama tunavyofahamu ajali tuliyopata imepelekea baadhi ya wachezaji takribani saba ambao kwa taarifa ya madaktari hawataweza kuendelea na michezo iliyobakia hivyo wameshauriwa wapumzike na ndio sababu kama timu tumewaongeza wachezaji watano kutoka katika kikosi chetu tulichonacho cha timu ya vijana,”alisema Juma .

Alieleza kuwa kiujumla wachezaji hao walioanza mazoezi wapo katika morali nzuri na wameahidi kupambana ili kupata matokeo katika michezo hiyo miwili iliyosalia ya ligi kwa kuanza na mchezo dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa kesho.

“Tumejipanga kuhakikisha vijana wetu wanafanya vizuri na tumeongea nao wametuahidi watatoa faraja kwa wenzao ambao hawatakuwa katika mchezo kutokana na kuwa bado ni majeruhi,”alisema Juma.

Aidha katika hatua nyingine alisema msimu ujao wa Polisi itatumia uwanja wa CCP-Moshi kwa mazoezi kwani ukarabati wa nyasi uko katika hatua nzuri na kuongeza kuwa wana mkakati wa kujenga uwanja.

Polisi Tanzania iko katika nafasi ya saba ikiwa imejikusanyia pointi 42 itamaliza mchezo wake wa mwisho dhidi ya Mwadui katika uwanja wake wa nyumbani wa Ushirika mwishoni mwa wiki hii.