Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 11 19Article 572878

Soccer News of Friday, 19 November 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Prisons yarudi kivingine, yapata ushindi wa kwanza

Tanzania Prisons yaichapa Mbeya Kwanza Tanzania Prisons yaichapa Mbeya Kwanza

Kwa mara ya kwanza Tanzania Prisons imeonja ushindi leo baada ya kuikachaza Mbeya Kwanza mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa leo Ijumaa, Novemba 19 uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa.

Kabla ya ushindi huo, Wajelajela hao walikuwa wamecheza mechi tano bila ushindi, wakipoteza tatu na sare mbili na kukaa mkiani kwa pointi mbili na leo imefanikiwa kubaki na alama tatu nyumbani.

Katika mchezo wa leo, Prisons walionesha mpira wa nguvu kwa kubutuabutua wakisaka mabao lakini walikumbana na upinzani mzito mbele ya wapinzani wao, Mbeya Kwanza.

Mbeya Kwanza ndio walitangulia kupata bao dakika ya 26 kupitia kwa Vedastus Mwihambi aliyejifungia wakati akiokoa hatari baada ya kukosa mawasiliano na Kipa wake, Benedict Haule.

Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuwapa presha wenyeji walioonekana kupagawa huku wakipambana kulazimisha mashambulizi na dakika ya 31 waliweza kusawazisha bao hilo kupitia kwa Dotto Shaban na kufanya dakika 45 za kwanza kumalizika kwa nguvu sawa.

Kipindi cha pili kila timu ilifanya mabadiliko kadhaa ikiwa ni mbinu za makocha kusaka matokeo mazuri, lakini Prisons ndio waliweza kunufaika zaidi.

Wakati wadau na mashabiki wakiamini mechi hiyo imelala kwa sare, Jeremiah Juma aliweza kuwanyanyua vitini kwa kuifungia bao la pili Prisons dakika ya 90 na kuihakikishia pointi tatu muhimu timu yake.

Hata hivyo, Mbeya Kwanza inakuwa mchezo wake wa kwanza kupoteza baada ya kufululiza sare katika michezo minne mfululizo.

Kwa matokeo hayo, Prisons inafikisha pointi tano, huku Mbeya Kwanza wakibaki na alama zao saba baada ya timu zote kushuka uwanjani mara sita.