Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 06Article 555640

Soccer News of Monday, 6 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Rivers United kuwajaza wachezaji wa Yanga Pesa

Kikosi cha Yanga Kikiendelea Kujifua Kikosi cha Yanga Kikiendelea Kujifua

Klabu Yanga Septemba 12, watakuwa na kibarua kizito cha kumenyana na Rivers United kutoka Nigeria katika mchezo wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaofanyika katika Uwanja wa Mkapa, Jijini Dar es Salaam.

Sasa katika kuhakikisha Yanga wanafanya vyema katika michuano ya kimataifa, uongozi wa timu hiyo kwa kushirikiana na wadhamini wao Kampuni ya GSM umeanza mipango mapema kwa kuweka mzigo wa maana ambao utaongeza hamasa ya ushindi kuelekea katika mchezo wao dhidi ya Rivers United ya nchini Nigeria.

Chanzo cha kuaminika kutoka klabu ya Yanga kimesema kuwa uongozi huo umeweka wazi mpango wa kuweka fedha za kutosha kwa ajili ya kuhamasisha ushindi kwa wachezaji kuelekea katika mchezo wao dhidi ya Rivers, jambo ambalo wanaamini litaongeza chachu ya ushindi kama ambavyo wamekuwa wakifanya katika michezo mingine mikubwa ya timu hiyo.

“Kama ambavyo imekuwa siku zote, siyo jambo geni kwetu ndani ya Yanga, imekuwa kawaida kwetu kuweka fedha kama motisha kwa wachezaji katika michezo mikubwa ili kuhamasisha ushindi.

“Hivyo hata katika mchezo wetu wa kimataifa dhidi ya wapinzani wetu Rivers itawekwa fedha ya kutosha ikiwa kama sehemu ya motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi.

“Wadhamini wetu wakiongozwa na GSM wamekuwa wakisimamia hilo mara kwa mara kuhakikisha tunafanya vyema na tayari, tunawashukuru kwani malengo yamekuwa ni kufika katika hatua nzuri katika michuano hii ya kimataifa na sio kushiriki tu".

“Lazima kuwe na mambo mengi ya kuweka hamasa ndani ya timu na hivyo ndio hufanywa na klabu nyingi za kisasa kutoa bonasi za ushindi kwa timu pindi inapopata ushindi,” kimesema chanzo hicho.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela akizungumza kuhusu kuwekwa kwa ahadi ya fedha kuelekea katika mchezo huo amesema:

“Bado ni mapema sana kuzungumzia suala la bonasi za mchezo huo hivyo kama kutakuwa au hazitakuepo mtafahamu huko mbeleni lakini kwa sasa bado ni mapema kusema,” amesema kiongozi huyo.