Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 15Article 551578

Habari za michezo of Sunday, 15 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ruksa kusajili 12 wa kigeni: TFF

Ruksa kusajili 12 wa kigeni: TFF Ruksa kusajili 12 wa kigeni: TFF

SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF), limeruhusu usajili wa wachezaji 12 wa kigeni kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu.

Rais wa TFF, Wallace Karia aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa, maamuzi hayo yalifikiwa kwenye kikao cha kamati ya utendaji kilichokutana jana.

Aidha Karia alisema, timu zimeruhusiwa kusajili wachezaji 40, kati ya hao 12 wa kimataifa ambapo kwenye mechi moja wataruhusiwa kucheza wanane.

Kanuni za msimu uliopita, zilikuwa zikiruhusu usajili wa wachezaji 30, kabla ya baadae Shirikisho la soka Afrika, Caf kuruhusu usajili wa wachezaji 40 kutokana na janga la Corona.

“Kutokana na tatizo la Corona, na sisi tumeona turuhusu usajili wa wachezaji 40, kati ya hao wachezaji 18 watakaocheza mechi, wa kigeni wanaruhusiwa wanane,” alisema.

Kanuni za ligi msimu uliopita,ziliruhusu usajili wa wachezaji 30, kati yao 10 wa kigeni na waliruhusiwa kucheza wote kwenye mechi moja.

“Usajili wa wachezaji umeongezwa kuhakikisha timu zinafanya vizuri hasa michuano ya kimataifa, ni jukumu lao kulinda nafasi nne tulizopata, kwa kufanya vizuri na kufika kuanzia hatua ya makundi,”alisema Karia akizizungumzia Simba, Yanga, Azam na Biashara zinazoshiriki michuano ya kimataifa.

Karia alisema ongezeko la wachezaji hao halitaathiri Ligi Kuu kwasababu wamepunguza idadi ya watakaoruhusiwa kuchezeshwa kutoka 10 msimu uliopita hadi nane ili kuwapa nafasi wachezaji wa ndani kupangwa.

Dirisha la usajili kwa timu zinzoshiriki michuano ya kimataifa ya Caf, linatarajiwa kufungwa leo saa 6:00.

Klabu za Tanzania zinazoshiriki michuano hiyo, zimekuwa kwenye harakati za usajili takriban wiki ya pili sasa.

Jana, Yanga ilifunga usajili wake kwa kumtambulisha beki Yannick Bangala baada ya Ijumaa kutambulisha nyota wengine wawili kutoka klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, ambao ni Djuma Shaban na winga Ducapel Moloko anayekwenda kuziba nafasi ya Tuisila Kisinda aliyeuzwa RS Berkane ya Morocco.

Kwa upande wa Simba, juzi walimtambulisha winga

Duncan Nyoni ambaye anatajwa kuwa mrithi wa Clatous Chama, na jana walimtambulisha Sadio Kanoute wa Mali anayecheza nafasi ya kiungo, Ousmane Sakho ambaye ni winga anatoka Senegal na mlinzi wa kati raia wa Kongo Hennock Inonga Baka ‘Varane’.

Simba ambao ndio wafalme wa soka Tanzania Bara, wapo Morocco kujiandaa na msimu mpya pamoja na michuano ya kimataifa na wamepangwa kuanza katika raundi ya kwanza kwa kucheza na mshindi kati ya Jwaneng Galaxy ya Botswana dhidi ya DFC Deme Arrondissement ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.