Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 17Article 551890

Soccer News of Tuesday, 17 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Sakho ampa mzuka Gomes, Varane akiwasha

Mchezaji mpya wa Simba, Pape Ousmane Sakho Mchezaji mpya wa Simba, Pape Ousmane Sakho

Kutua kwa kiungo fundi wa mpira, Pape Ousmane Sakho kutoka Senegal ndani ya kambi ya Simba iliyopo Morocco, kumempa mzuka mwingi, Kocha Didier Gomes, kwani imemrahisishia kazi katika kuwapika vijana wake kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano.

Sakho amesajiliwa na kutambulishwa juzi, tayari yupo Rabat kwenye kambi ya timu hiyo na inaelezwa ujio wake umekamilisha kikosi kizima na kuongeza kasi ya mazoezi.

Simba iliondoka nchini kwa awamu, jambo linalotajwa kumchelewesha kocha Gomes kuanza rasmi programu yake ya mazoezi kwenye kambi hiyo, lakini kutua kwa kiungo mshambuliaji huyo anayetajwa kuziba nafasi ya Clatous Chama aliyeuzwa RS Berkane ya Morocco, kumempa furaha kubwa kocha huyo.

Mmoja ya wachezaji wa Simba waliopo kambini Morocco amedokezsa kuwa, walikuwa wanapiga sana tizi la gym na mazoezi zaidi ya viungo kwa ajili ya kujiweka fiti.

“Alikuwa anasubiri timu yote ifike ndipo ratiba rasmi ikiwamo kucheza mechi za kirafiki ianze,” alisema mmoja wa wachezaji wa timu hiyo kutoka Morocco jana na kuongeza walikuwa wakifanya mazoezi ya kawaida wakati wakiwasubiri wachezaji wengine ili kuanza programu rasmi ya pamoja.

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema kwamba tayari timu yote imewasili Morocco kambini.

“Wachezaji wote wako Morocco tayari hadi yule kiungo Msenegal, timu itakuwa kambini nchini humo kwa muda mrefu kwa kuwa hatuna haraka yoyote ya kuwahi kuirejesha nchini, ukizingatia ligi ya mabingwa Simba tunaanzia raundi ya pili,” amesema Mangungu na kuongeza;

“Mikakati yetu ni kufanya mazoezi ya nguvu, kujipanga ipasavyo kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi msimu ujao kwenye Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa, hivyo kocha ndiye ataamua ni muda gani watautumia kwenye kambi hiyo kabla ya kurejea nchini.”

Kutoka Morocco mmoja wa wachezaji amesema kocha Gomes alikuwa akisubiri wachezaji wote watimie ndipo aanze programu rasmi ya pamoja kama timu.

“Jumanne bila shaka tutajua ni timu ipi tuanze kucheza nayo mechi ya kirafiki na ratiba yote ya huku, ukiachilia mbali mazoezi ambayo tunaendelea kufanya tangu msafara wa kwanza ulipowasili mjini Rabat wiki iliyopita,” amesema.

Amesema tangu wamewasili nchini humo wamekuwa katika kipindi bora cha mazoezi katika kambi ambayo ni tulivu na inawapa mazingira rafiki ya kujifua kwa ufasaha.

“Kwa mazingira ya kambi hii, tukirejea nyumbani Simba itakuwa ni moto mwingine, zaidi ya ile ambayo imekuwa bingwa mara nne mfululizo wa Ligi Kuu na ile ya Ligi ya Mabingwa msimu uliokwisha. Kambi yetu ni habari nyingine kabisa,” amesema.

Amesema wachezaji wapya waliojiunga na timu hiyo wameongeza hamasa na kwa namna walivyoanza hakuna shaka watakuwa na mchango mkubwa kwenye timu msimu ujao.

Simba imepangwa kuanza mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika katika raundi ya pili dhidi ya mshindi kati ya Jwaneng Galaxy ya Botswana na DFC Beme ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, lakini wakiwa na kibarua cha kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tano mfululizo na Kombe la ASFC kwa msimu wa tatu.