Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 15Article 542773

Habari za michezo of Tuesday, 15 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Sarakasi Uchaguzi Mkuu TFF

Sarakasi Uchaguzi Mkuu TFF Sarakasi Uchaguzi Mkuu TFF

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema mchakato wa mabadiliko ya Katiba ulianza mwaka 2018 na wala haukulenga kumpendelea mgombea yeyote kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 7, mwaka huu jijini Tanga.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred alipozungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam na kusema Katiba hiyo ilipitishwa mwaka 2019 na Mkutano Mkuu wa TFF uliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu na baadaye ikapelekwa kwa Msajili wa Vyama vya Michezo na Klabu kupitishwa.

Kidao alisema mchakato wa uchaguzi uko chini ya Kamati ya Uchaguzi na kuwataka watu wasiingilie kwa kutaka kupeleka mambo nje ya mamlaka ambayo haihusiki na mpira wa miguu ili kuepuka madhara ya kufungiwa na Fifa.

"Kuhusu elimu tukumbuke miaka ya nyuma kulikuwa na kufungiana fungiana kutokana na viongozi kutokuwa na elimu na mchakato wa elimu ulifanywa kuanzia mwaka 2006."

"Hata kipengele cha kuwadhamini wagombea TFF hawahusiki na suala hilo kwa sababu ni la mgombea na wanachama, kama shirikisho tuliwajulisha wanachama wetu mgombea urais anatakiwa awe na wadhamini watano na mjumbe awe na mdhamini mmoja," alisema Kidao.

Alisema wadau wanatakiwa kuheshimu mchakato huo na kuiachia Kamati ya Uchanguzi kufanya kazi yake, wasikubali kuingia katika migogoro ambayo itawaweka katika wakati mgumu wa nchini kufungiwa na kushindwa kushiriki michuano ya kimataifa kwa ngazi ya taifa na klabu pia.

Katika hatua nyingine, mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa shirikisho hilo, Abdallah Bulembo alisema amewasilisha barua FIFA kupinga waliocheza mpira kuenguliwa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi kutokana na kigezo cha elimu.

Alisema Mei 5 aliwasilisha barua Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo akiitaarifu uchaguzi wa TFF unakaribia na kuna baadhi ya vipengele vya kanuni katika Katiba vinahitaji kufanyiwa marekebisho, lakini mwezi umepita sasa haijajibu.

Alisema moja ya vipengele hivyo ni kuwanyima haki wachezaji waliocheza mpira kuwania nafasi ya urais kwa kigezo cha kuwa na elimu ya shahada, lakini serikali kupitia wizara haijatoa jibu lolote.

"Juni 9, mwaka huu niliwasilisha barua FIFA nikiwaeleza kanuni za TFF zina shida, bado sijapata jibu lolote ila nina imani nitajibiwa na pengine watakuja na vipengele virekebishwe ili uchaguzi uwe huru na haki, kwani haiwezekani mtu aliyecheza soka Tanzania asiruhusiwe kuongoza mpira kwa kigezo cha elimu,” alisema Bulembo na kuongeza:

"Ninachozungumza isiwe ajenda kati yangu na Rais Wallace Karia, bali ni suala la wachezaji kutengwa na kanuni za wachezaji waliocheza soka kutopewa nafasi ya kugombea kwa sababu ya ukosefu wa shahada, mfano kwa Mbwana Samatta anayecheza soka Ulaya endapo atarudi hataweza kugombea kutokana na kigezo hicho," alisema Bulembo.

Alisema kigezo cha elimu kibaki kwa watendaji wa kuajiriwa, lakini kwa nafasi za kuchaguliwa kiondolewe kwani kinafanya wachezaji mpira wasiongoze na kuhoji jasho lao wakalitumikie wapi, hivyo atapambana hadi haki ipatikane.

Pia alisema kipengele kingine cha Rais wa TFF kumteua makamu wake kifanyiwe marekebisho kwani kwa sasa anateuliwa badala ya kuchaguliwa na wanachama kama ilivyokuwa awali na baadae waende kwenye uchaguzi.

Bulembo alifika mbali na kuhoji mbona Fifa na Caf hakuna vigezo vya elimu na kuuliza kwa nini TFF inakuwa na kigezo cha kuwabana watu.

Naye mgombea wa urais wa shirikisho hilo, Ally Saleh 'Alberto' alisema ameiandikia barua Wizara ya Michezo na Msajili wa Vyama ili kushughulikia mapungufu yaliyomo kwenye Katiba na kanuni za uchaguzi wa TFF kwa sababu hakuna mwanachama kutoka Zanzibar.

"Hakuna chama chochote cha mpira wa miguu visiwani Zanzibar ambacho ni mwanachama wa TFF, hali ambayo inawanyima uhuru kugombea kwa kukosa wadhamini," alisema Saleh.

Wagombea wa urais waliochukua fomu na kurejesha ni Karia, Ally Mayay, Ally Saleh, Hawa Mniga, Oscar Oscar na Evans Mgeusa.

Waliochukua fomu na kushindwa kurejesha ni Abbas Tarimba, Deogratius Mutungi, Rahim Kangezi na Zahor Mohammed Haji.

Karia ambaye anatetea nafasi yake, aliingia madarakani Agosti 12, 2017 katika uchaguzi uliofanyika jijini Dodoma, ambapo alipata kura 95 kati ya kura 127, akifuatiwa na Ally Mayay aliyepata kura tisa sawa na Shija Richard.