Uko hapa: NyumbaniMichezo2022 01 12Article 585145

Soccer News of Wednesday, 12 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Simba Queens yajifua Nyamagana, Nkoma aahidi ushindi

Simba Queens wakiendelea na mazoezi Simba Queens wakiendelea na mazoezi

Timu ya Simba Queens imefanya maandalizi ya mwisho katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo wake wa Ligi Kuu ya Wanawake dhidi ya Alliance Girls.

Simba Queens itashuka uwanjani saa 10 jioni kukipiga na wenyeji wao Alliance Girls kwenye Uwanja wa Nyamagana katika mchezo wa raundi ya tano ya Ligi ya Wanawake.

Vinara hao wa Ligi walifika uwanjani hapo saa tatu asubuhi na kuanza mazoezi yao chini ya Kocha Mkuu Sebastian Nkoma.

Nkoma amewasisitiza vijana wake kucheza soka la utulivu, kugongeana pasi, kupiga mashuti, ujanja katika upigaji wa mipira ya faulo karibu na lango la wapinzani pamoja na upigaji penalti.

Kikosi hicho ambacho kinaongoza Ligi kikiwa na pointi 12 katika mechi nne kikiwa hakijapoteza mchezo kimejifua na nyota wake 15 walioambatana na timu hiyo jijini Mwanza kwa basi huku nyota wengine wakiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa na majeruhi.

Akieleza maandalizi yake kuelekea mchezo wa kesho, Nkoma amesema wamechukua tahadhari zote kwa sababu ni mchezo wa kwanza nje ya Dar es Salaam hivyo wamejipanga kuendelea kuvuna pointi tatu na kung'ang'ania kileleni.

"Nimekuja na wachezaji wachache lakini naamini watanipa matokeo kwa maandalizi ambayo tumefanya, tunafahamu ligi ni ngumu timu zinazidi kuimarika nasi tunajiweka vyema ili tuwe juu," amesema Nkoma.

Baada ya mchezo huo, Simba Queens itashuka tena kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza Januari 16 kuwakabili TSC Queens katika mwendelezo wa ligi hiyo.