Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 09Article 541684

Habari za michezo of Wednesday, 9 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Simba, Simba, Yanga zamuwania beki AS Vita

KLABU ya soka ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imesema ipo tayari kumuachia mlinzi wake wa kulia na nahodha wa timu hiyo, Djuma Shabani ajiunge na timu yoyote itakayotoa dau nono litakalowashawishi.

Simba na Yanga ni miongoni mwa timu ambazo zinasaka saini ya mlinzi huyo, ambaye amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu hiyo, hasa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Raul Shungu akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kwa njia ya mtandao alithibitisha jana kuwa Yanga na Simba zimeonesha nia ya kumtaka mchezaji huyo, lakini hakuna iliyowasilisha ofa mezani.

“Djuma Shabani bado ni mchezaji wetu halali sababu mpaka sasa hakuna timu ambayo imeleta ofa kwa ajili ya kuhitaji huduma yake, awali klabu ya Simba ilikuwa ikifanya mazungumzo naye na hivi sasa Yanga wapo kwenye mazungumzo naye, lakini hawajafikia makubaliano ya kusaini mkataba naye,” alisema Shungu.

Kocha huyo aliyewahi kuifundisha, Yanga kwa mafanikio makubwa alisema wao hawana pingamizi kwa mchezaji huyo na wapo tayari kumuachia endapo moja wapo kati ya miamba hiyo ya soka ya Tanzania itafikia makubaliano naye ya kimkataba na mshahara.

Alisema mpira siku hizi ni ajira hivyo hawawezi kumbania mchezaji huyo hata kama atakuwa na mkataba wa muda mrefu ispokuwa wanachotaka wao ni timu inayomuhitaji kufuata taratibu zinazotakiwa kwa ajili ya kumalizana nao.

Awali, Simba ilitajwa kuwa na mpango wa kumchukua mchezaji huyo baada ya kuonesha kiwango bora kwenye pambano lao la awali la hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambalo lilipigwa Kinshasa na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Hivi karibuni watani zao Yanga nao wamekuwa wakihusishwa na taarifa za kumalizana na beki huyo ili msimu ujao aweze kuwatumikia wana Jangwani hao, lakini kwa mujibu wa Shungu mpaka sasa hakuna timu ambayo imeshajihakikishia kupata huduma ya beki huyo mwenye uwezo mkubwa.