Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 22Article 558970

Habari za michezo of Wednesday, 22 September 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Simba: Waleteni Wabotswana

Simba: Waleteni Wabotswana Simba: Waleteni Wabotswana

SIMBA imeshajua wapinzani wake katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambao watakuwa ni Jwaneng Galaxy ya Botswana ambapo mshindi wa mechi mbili baina ya timu hizo atatinga hatua ya makundi.

Wawakilishi hao wa Tanzania wataanzia ugenini Botswana Oktoba 15 au 16 na mechi ya marudiano itachezwa Dar es Salaam wiki moja baadaye.

Wakati Simba wakianza kujipanga na mechi hizo mbili dhidi ya Jwaneng Galaxy, rekodi ya mechi zilizopita dhidi ya timu za Kusini mwa Afrika na Botswana zinaweza kuwapa matumaini wawakilishi hao wa Tanzania kusonga mbele kuingia hatua inayofuata

Simba imekuwa na historia ya kufanya vizuri mara kwa mara inapokutana na timu kutoka ukanda wa Kusini mwa Afrika ingawa mara kadhaa huangukia pua

Takwimu zinaonyesha katika michezo 55 ya mashindano ya klabu Afrika, Simba imeibuka na ushindi mara 29, kutoka sare 11 na kupoteza jumla ya michezo 15.

Kana kwamba haitoshi, Simba imefanikiwa nyavu mara 85 huku ikiruhusu nyavu zake kutingishwa mara 55 ikiwa ni wastani wa bao moja inayoruhusu katika kile mchezo.

Hata hivyo imekuwa haifui dafu mara kwa mara katika mechi za ugenini kwani katika mechi 28 ilizocheza dhidi ya timu za Kusini mwa Afrika, Simba imeibuka na ushindi mara nane, kutoka sare nane na kupoteza mechi 12.

Simba imekuwa moto wa kuotea mbali zaidi inapokuwa nyumbani kwani kati ya michezo 27 iliyocheza dhidi ya wapinzani kutoka nchi zilizo Kusini mwa Afrika, imeibuka na ushindi mara 21, ikitoka sare mara tatu na kupoteza mechi tatu tu.

Ubabe huo kwa Simba upo hata dhidi ya timu kutoka Botswana kwani hapo awali, imeshakutana na timu za huko mara mbili na kuibuka na ushindi katika mechi zote.

Timu ya Botswana ambayo Simba imewahi kukutana nayo ni Botswana Defence Force XI ambapo walicheza nayo mwaka 2003 katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo waliibuka na ushindi nyumbani na ugenini na kusonga mbele

Simba ilishinda katika mchezo wa kwanza nyumbani kwa bao 1-0 na kisha ikapata ushindi wa mabao 3-1 ugenini huko Gaborone, Botswana.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema licha ya historia nzuri ya timu yake, mechi dhidi ya Jwaneng itakuwa ngumu na watajipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

“Hakuna mechi rahisi katika haya mashindano na kila timu inafanya maandalizi hivyo tunapaswa kuwa makini ili tuweze kupata matokeo mazuri ambayo yatatupeleka katika hatua inayofuata.

Tuna wachezaji wazuri ambao wengi wana uzoefu wa mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo naamini watakuwa chachu kwetu kufanya vizuri,” alisema Gomes.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Musa Hassan Mgosi alisema kitakachowabeba Simba ni maandalizi na ubora wa kikosi.

“Rekodi hazichezi na haziwezi kukupa matokeo mazuri kama haujafanya maandalizi ya kutosha. Mimi naipa nafasi Simba ya kufanya vizuri kwa sababu inafanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.

Soka kwa sasa limebadilika na hakuna timu nyepesi katika mashindano ya Afrika. Wito wangu kwa wachezaji ni kucheza kwa kujitolea ili tufikie mafanikio ya msimu uliopita au zaidi ya hapo,” alisema Mgosi.