Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 22Article 559006

Habari za michezo of Wednesday, 22 September 2021

Chanzo: ippmedia.com

Simba: Yanga haitoki, Ngao Jamii mali yetu

Simba: Yanga haitoki, Ngao Jamii mali yetu Simba: Yanga haitoki, Ngao Jamii mali yetu

WAKATI homa ya mechi ya watani wa jadi ikizidi kupanda huku Shirikisho la Soka nchini (TFF), likitangaza viingilio vya mchezo huo maalum kwa ajili ya kukaribisha msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2021/22, mabingwa wa soka nchini, Simba, wamesema wapinzani wao, Yanga wasahau kutwaa Ngao ya Jamii kwa sababu kwa sasa wanaichukuliwa kama ni mali yao.

Vigogo hivyo vya soka nchini, vitakutana Jumamosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na baada ya mchezo huo wa kuwania Ngao ya Jamii, msimu mpya wa Ligi Kuu 2021/22, utakuwa umezinduliwa rasmi ambapo utaanza Septemba 27, mwaka huu.

Mratibu wa Klabu ya Simba, Abbas Ally, amesema kwa sasa timu yao imesharejea kambini baada ya mapumziko ya siku moja, lilipomalizika Tamasha la Simba Day na sasa ni rasmi wamefungua msimu mpya wa mashindano.

"Sisi tumeshaichukua Ngao ya Jamii mara mbili mfululizo. Ni mali yetu sasa, kwa hiyo hatuwezi kuiacha. Hatuwezi kumuachia mtu yeyote Ngao ya Jamii," alisema mratibu huyo.

Alisema wanachoshukuru ni kwamba baada ya kumalizika mechi dhidi ya TP Mazembe na kuchapwa bao 1-0 Jumapili iliyopita, hapakuwa na mchezaji yeyote majeruhi, hivyo timu inakwenda kuanza msimu ikiwa na wachezaji wote 32 iliyowasajili.

"Hii ni faraja kwetu na kocha atakuwa na chaguo pana zaidi kwani atakuwa na wachezaji wake wote, kwa sababu tuna mechi mfululizo. Tukitoka kucheza dhidi ya Yanga Jumamosi, tuna mechi nyingine Musoma na Dodoma," alisema mratibu huyo.

Akizungumzia maandalizi alisema kwa sasa kocha anarekebisha upungufu aliyouona kwenye mechi zilizopita.

"Si mechi ya TP Mazembe peke yake, hata zile mechi za kirafiki tulizocheza Morocco na Arusha nazo pia zilikuwa na makosa kadhaa ambayo yanahitaji kurekebishwa na wakati wake ni huu," alisema.

Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Hassan Bumbuli, alisema wamerejea na wanaendelea kujiandaa vizuri kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mechi ya hiyo.

"Baada ya mchezo wetu dhidi ya Rivers United kule Port Harcourt, Nigeria, wachezaji wote wamehamishia mawazo yao kwenye 'derby' wikiendi hii, mechi hii ndio mwanzo wetu wa kuanza vema kwenye ligi na kutwaa mataji na kufikia malengo yetu ya kurejesha heshima ya klabu hii," alisema Bumbuli.

Alisema wachezaji wako fiti na nyota watatu ambao hawakucheza dhidi ya Rivers United, Fiston Mayele, Shaaban Djuma na Khalid Aucho watakuwapo kwenye mchezo huo.

Wakati huo huo, Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo, akitangaza viingilo vya mechi hiyo, alisema jukwaa la VIP A litakuwa ni kwa ajili ya watu maalum, huku VIP B kiingilio kikiwa ni Sh. 30,000, VIP C na viti vya rangi ya machungwa Sh. 20,000 na viti vya bluu na kijani Sh. 10,000.

Alisema wametaja viingilio hivyo mapema ili mashabiki na wadau wa soka kujiandaa na ndani ya hizi siku mbili wataweka wazi vituo vitakavyouzwa tiketi hizo.

"Kwa upande wa TFF maandalizi yanaenda vizuri, kuelekea mchezo huo na siku mbili kabla ya mechi tutawaeleza vituo vya kununua tiketi za mechi hiyo ya ufunguzi wa ligi," alisema Ndimbo.