Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 11Article 556936

Habari za michezo of Saturday, 11 September 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Simba kuanza na DTB kisha Namungo

Simba kuanza na DTB kisha Namungo Simba kuanza na DTB kisha Namungo

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua vikali kambini jijini Arusha, ikiwa ni maandalizi ya mwisho mwisho kabla ya kuja kuliamsha ndani ya Tamasha la Simba Day, huku kocha mkuu wa timu hiyo akitaka mechi mbili tu za mwisho amalize kazi mapema kabla ya kuivaa TP Mazembe na kuigeukia Yanga.

Tangu Simba irejee kutoka Rabat, Morocco ilikoenda kupiga kambi ya wiki mbili, Gomes alikuwa akiwapigisha tizi la gym vijana wake na siku moja kabla ya kutimkia Karatu, Arusha walipopiga kambi walikiwasha kidogo pale Uwanja wa Uhuru na sasa wanalishwa mbinu kabla ya kuja kuanza mambo kwa msimu mpya.

Inaelezwa Gomes baada ya kuwapa mazoezi mengi ya nguvu wachezaji wake kwa siku awamu mbili wakiwa Rabat akilenga zaidi kuandaa miili kwa ajili ya kushindana msimu ujao, kwa sasa ameanza kuwapa mazoezi mengi ya mbinu na kucheza zaidi na wameanza kulifanya hilo kambini Arusha.

Katika mazoezi hayo Gomes amekuwa akikomalia zaidi mbinu mbalimbali kama kufunga, kushambulia kupitia viungo pamoja na mabeki wa pembeni, kukaba na kuzuia mashambulizi aina mbalimbali, kupiga frii-kiki, penalti, kona na mengineyo mengi.

Inaelezwa Gomes amekuwa mkali katika mazoezi hayo na wala hataki mzaha kutoka kwa mchezaji wake yeyote kwani yule ambaye amekuwa akishindwa kufanya vizuri huwa anasimamisha na kuanza kumuelekeza jambo la kufanya wakati huo.

Katika mazoezi hayo wachezaji wengi wamekuwa wakifanya vizuri kutokana na majukumu yao lakini inaelezwa kuna nyota watatu wamekuwa wakifunika zaidi haswa katika mazoezi ya kucheza timu mbili tofauti ambao ni Pape Ousmane Sakho, Sadio Kanoute na Ibrahim Ajibu.

Chanzo kutoka ndani ya kambi ya Simba kinasema tangu akiwa Rabat, Ajibu ameonekana kubadilika akiwa hana mzaha kwenye kutimiza majukumu yake kwani amekuwa akifunga mabao ya aina mbalimbali, kuhusika katika mabao ikiwemo kutoa pasi za mwisho pamoja na mambo mengine ambayo katika misimu miwili iliyopita hakuwa nayo.

Pia amekuwa akishirikiana vyema na Sakho na inaelezwa kama akiendelea na moto huo ni wazi ataongeza makali ya ushindani wa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, pia ikidaiwa ni kubanwa na mkataba wake mpya wa miaka miwili uliokuwa na vipengele vigumu ikiwemo kuboresha kiwango.

MECHI MBILI TU

Baada ya juzi kucheza mchezo wao wa kwanza wa kirafiki nchini dhidi ya Coastal Union na kumalizika kwa suluhu, kocha Gomes ametaka mechi nyingine mbili za mwisho kabla ya kwenda kuvaana na TP Mazembe kwenye Kilele cha Tamasha la Simba Day kitakachofanyika Septemba 19.

Simba imepanga kupiga mechi mbili hizo za mwisho kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya tamasha lao dhidi ya DTB inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (Championship) na baada ya hapo watamaliza na Namungo.

“Kocha anaamini mechi hizo zitamsaidia kupata picha nzuri zaidi kuelekea msimu mpya kabla ya kuvaana na Mazembe itakayowaongezea kitu kisha kuwakabili Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayochezwa wiki moja baada ya tamasha,” kilisema chanzo hicho kutoka Simba.

Aidha, imeelezwa kocha Gomes amewataka wachezaji waliokuwa katika majukumu ya timu zao za taifa baada ya kucheza mechi za mwisho kurejea kambini kwa haraka ili kuungana na wenzao katika maandalizi hayo.

Inaelezwa jioni ya jana (Alhamisi), wachezaji wa Simba waliokuwa katika kikosi cha Taifa Stars waliwasili katika kambi hiyo na waliungana na wenzao kwa ajili ya maandalizi ya kutosha.

Wachezaji hao sita waliokuwa Stars ni Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin ambao wote walianza katika kikosi cha kwanza kwenye mechi ya Madagascar na Israel Patrick.

Mratibu wa Simba, Abbas Selemani alisema kambi yao inaendelea vizuri kutokana na wachezaji wote wapo katika morali na wote waliokuwa katika timu zao za taifa watarejea haraka kambini ili kujiunga na wenzao.

“Kocha anataka kuwepo na wachezaji wote ili kupata muunganiko haswa kwa wale waliokuwepo msimu uliopita na sasa ili kupata fursa kuzoeana kwa haraka na kwenda kuleta ushindani katika mechi zetu,” alisema Selemani.