Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 05 30Article 540649

xxxxxxxxxxx of Sunday, 30 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Simba yaanza kula viporo

VINARA wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara Simba wamekula kiporo chao vizuri dhidi ya Namungo baada ya kuwachapa mabao 3-1 kwenye uwanja wa Majaliwa,Lindi jana.

Mabao yalifungwa na Styve Nzigamasabo kwa Namungo huku yale ya Simba yakifungwa na Chris Mugalu, John Bocco na Bernard Morrison.

Ushindi huo unaifanya Simba kuendelea kujikita kileleni kwa kufikisha pointi 64 katika michezo 26 na kumwacha mpinzani wake Yanga kwa tofauti ya pointi tatu katika michezo 29.

Namungo ilitangulia kupata bao la kuongoza dakika ya 21 likifungwa na Nzigamasabo baada ya kupokea pasi ya Reliant Lusajo. Bao hilo lilidumu hadi timu hizo zinakwenda mapumziko.

Kipindi cha pili Kocha Didier Gomes wa Simba alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mzamiru Yassin, Meddie Kagere na Rally Bwalya dakika ya 45, 57 na 71 na kuingia Morrison, Bocco na Hassan Dilunga.

Mabadiliko hayo yalisaidia Simba kuongeza kasi ya mashambulizi langoni kwa wapinzani ambapo dakika ya 78 Mugalu alisawazisha bao baada ya pasi nzuri ya Shomari Kapombe.

Kitendo cha kusawazisha kiliwafanya Simba kujiamini na kumiminika langoni kwa Namungo kila mara kama nyuki na dakika ya 83 Bocco alifunga bao zuri la pili kwa kichwa baada ya kupokea krosi ya Mugalu.

Dakika nne baadaye Simba iliongeza bao la tatu likifungwa kutoka katikati ya uwanja na Morrison.

Simba ilimiliki mpira tofauti na wapinzani wao Namungo walioonekana kuchoka na kuzidiwa hasa kipindi cha pili.

Join our Newsletter