Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 08Article 556060

Habari za michezo of Wednesday, 8 September 2021

Chanzo: ippmedia.com

Simba yaitaka Tusker ikiisubiri TP Mazembe

Simba yaitaka Tusker ikiisubiri TP Mazembe Simba yaitaka Tusker ikiisubiri TP Mazembe

NI rasmi sasa Klabu ya Simba itajaribu mitambo yake na kutoa burudani kwa mashabiki na wanachama wao, itakaposhuka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, kucheza mechi ya kirafiki katika kikele cha Tamasha la Simba Day.

Katika kujiandaa na tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Septemba 19, mwaka huu, Simba imepanga kupata mechi moja ya kirafiki ya kimataifa ikiwa jijini Arusha, huku ikielezwa mipango inafanyika kucheza na Tusker FC ya Kenya.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alisema katika kuadhimisha Simba Day, timu hiyo itacheza na mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe.

Alisema wamekamilisha taratibu zote za kuwaalika na sasa ni rasmi TP Mazembe ya DR Congo, watakuwa wageni wa Simba siku hiyo muhimu ya kilele cha tamasha lao.

"Nifuraha kuwatangazia Wanasimba na Watanzania wote kwa ujumla kwamba tutacheza na TP Mazembe Simba Day, ni moja ya timu zenye heshima kubwa barani Afrika pia ni heshima kwa Simba kupata fursa ya kucheza nayo hapa nchini," alisema Gonzalez.

Alisema lilikuwa lengo la uongozi na benchi la ufundi kuhakikisha Simba inapata timu nzuri ili Kocha Mkuu, Didier Gomes kujua upungufu na ubora wa kikosi chake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema wachezaji wote 21 waliopo kambini jijini Arusha wako kwenye hali nzuri na wale wageni wamezoeana na wenzao pamoja na mazingira ya timu.

Alisema waliendelea na mazoezi ya mara mbili kwa siku, asubuhi na jioni na kwamba kikubwa kwao ni kuendelea kutafuta stamina pamoja na mbinu za uwanjani kwa muda ambao watakuwapo kambini hapo huku wakitarajia kucheza mechi za kirafiki.