Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 13Article 557077

Habari za michezo of Monday, 13 September 2021

Chanzo: eatv.tv

Sports Countdown, Salah aweka rekodi, Yanga hoi

Deniil Medvedev, bingwa wa US Open Deniil Medvedev, bingwa wa US Open

6 - Ni mabao yaliyofungwa kwenye michezo mitatu iliyowahusisha wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa Wikiendi iliyopita ambapo klabu ya Biashara United Mara imeingia kwenye vitabu vya historia baada ya kupata ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Dikhil ya Djibout, Azam iliifunga Horseed ya Somalia 3-1 kwenye michezo ya mtoano ya awali kuwania kufuzu makundi ya michuano ya Kombe la shirikisho Barani Afrika wakati Yanga yalipewa kibano cha bao 1-0 kwenye dimba lake la Nyumbani la BW Mkapa na Rivers United ya Nigeria kwenye mchezo wa mtoano wa awali kuwania kufuzu makundi ya michuano ya klabu bingwa Afrika.

Kipigo hicho kwa Yanga ni kipigo cha tatu mfululizo kwenye michezo yake 6 rasmi kwa maana ya kutoka sare michezo 3 na kufungwa michezo  mitatu.

Kwa upande wa visiwani Zanzibar,  KMKM alifungwa 2-0 na Ittihad ya Misri.

5 - Ni idadi ya wachezaji nyota walioonesha viwango bora na kuweka rekodi za kibabe kwenye michezo ya ligi kuu mbali mbali zilizopigwa wikiendi iliyoisha. 

Wachezaji hao ni, CR7 ambaye alifunga mabao 2 kwenye mchezo wake wa kwanza wa EPL kwenye ushindi wa 4-1 kwa Man Utd dhidi ya Newcastle tokea ajiunge tena na Man Utd akitokea Juventus ya Italia. Bruno Fernandes wa Utd pia alifunga moja ya bao kwenye mchezo huo na kuweka rekodi ya kuhusika kwenye mabao mengi zaidi 48 kwenye EPL tokea atue Man Utd 1 Feb 2020 wakati Paul Pogba akitoa assist 2 kwenye mchezo huo na kuzipiku jumla ya assist zake za misimu miwili iliyopita kwa kufikisha jumla ya Assist 7 kwa sasa.

Nchini Ujerumani stori iliibwa tena na mfungaji jini, Braut Erling Haaland ambaye alifunga bao 2 kwenye ushindi wa 4-3 wa B.Dortmund dhidi ya Bayer Leverkusen na kufikisha mabao 65 kwenye michezo 65 ya timu hiyo na kuwa mtu wa kwanza kufanya hivyo.

Wa mwisho ni Kiberenge Mo salah wa Liverpool ambaye alifunga bao 1 kwenye ushindi wa 3-0 wa Liverpool dhidi ya Leeds Utd na kufikisha bao lake la 100 kwenye EPL na kuwa mchezaji wa tano kufikisha mabao 100 kwa kutumia michezo michache michezo 162.

4 - Ni idadi ya miaka ambayo mshambuliaji Mtanzania, Mbwana Sammatta aliitumikia klabu ya KRC Genk ya Ubeligiji kwa kucheza michezo 191, kufunga mabao 76 na ku-assist mabao 20 kuanzia msimu wa mwaka 2016-2020 kabla hajajiunga na Aston Villa ya EPL Januari 2020 ambao walimuuza Fenerbhance ya Uturuki mwaka jana na hatimaye Fenerbhance kumtoa nyota huyo kwa mkopo wa miaka 2 kwenye klabu ya Royal Antwerp ya Ubeligiji mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

Sammatta amecheza mchezo wake wa kwanza na klabu yake mpya Jumamosi ya Septemba 11 mwaka huu akiingia dk 56' kutokea benchi alipochukua nafasi ya winga Manuela Benson mwenye asili ya Angola.

Royal Antwerp iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya EUPEN na sasa ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi kuu nchini humo maarufu 'Jupiler Pro League' ikiwa na alama 8 baada ya kucheza michezo 6.

3 - Ni dakika zilizoongezwa kwenye mchezo wa ligi ya Italia Seria A kati ya AS Roma dhidi ya Sassoulo baada ya dakika 90 kumalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu kwa sare ya 1-1.

AS Roma ilifanikiwa kufunga bao la pili baada ya dakika 1' ya nyongeza kupita bao lililofungwa kikatili na winga wake hatari Stephan El Sharawy na kuwafanya watakatifu hao wa jiji la Roma kukwea kileleni mwa Serie A wakiwa na alama 9 baada ya ushindi wa michezo yote 3 waliyocheza ya ligi hiyo.

Ushindi huo pia ni wakihistoria kwa kocha Jose Mourinho kwani ametimiza mchezo wake wa 1,000 tokea awe kocha na kushinda michezo 639 na kutwaa makombe 25 akiwa na vilabu vya FC Porto, Chelsea, Inter Milan, Real Madrid na Manchester United huku akivinoa pia vilabu vya Benifica, Tottenham Hotspurs na AS Roma ya sasa bila kubeba makombe.

2 - Ni miaka iliyopita Mrusi, Deniil Medvedev atinge fainali yake ya kwanza ya grand slam na kupoteza mbele ya Rafael Nadal kwenye fainali ya US Open iliyomfanya Nadal afikishe Grand Slam 19 huku Medvedev akiumizwa sana kufuatia kupoteza fainali hiyo na kujiapiza kutumia maumivu hayo kama hamasa ya kuusaka ubingwa huo.

Maneno ya Medvedev hatimaye yametimia kwani usiku wa kuamkia leo ameibuka kuwa bingwa wa US Open ikiwa ni ubingwa wake wa kwanza wa Grand Slam kwa kumfunga Mserbia Novak Djokovic anayeshikilia nafasi ya 1 kwa ubora duniani kwenye tennis upande wa wanaume kwa seti seti 6-4, 6-4 na 6-4.

Licha ya kupoteza fainali lakini Djokovic alipewa heshima na watazamaji wa mchezo huo kwa kumpigia makofi mengi jambo lililomfanya atokwe na machozi baada ya kipigo hicho kumfanya ashindwe kuweka rekodi ya kuwa mcheza tennis mwenye grand slam nyingi 21 kwenye historia na kuwapiku Rafael Nadal na Rodger Federer pamoja na kubeba makombe yote ya kalenda ya mwaka ya grand slam tokea 1969.

Kwa upande wa Wanawake, Emma Raducanu amemfunga Leylah Fernandez na kuwa bingwa wa US Open kwa mara ya kwanza na kuweka rekodi ya kuwa bingwa wa kwanza mwenye umri mdogo 18 tokea Maria Sharapova 2004. Emma amepata paundi mil 1 = 3Bil Tshs.

1 - Ni idadi ya wiki iliyopita tokea Max Vesterpen aibuke kuwa mshindi wa Mbio magari za Belgium Grand Prix kwa kumpiku Lewis Hamilton wa timu ya Mercedes kufuatia mvua kali iliyopelekea mashindano hayo kuhairishwa kwenye mzunguko wa pili na Vesterpen kupewa ushindi kikanuni kwa kuwa alikuwa aliyekuwa anaongoza mbio hizo.

Wawili hao wameshindwa kuibuka na ushindi kwenye mashindano ya mbio za magari za Italian Grand Prix baada ya gari Vesterpen kugonga gari la Lewis Hamilton tukio lililopelekea  dereva wa timu ya McLaren Daniel Ricciardo kuwapita na kuibuka mshindi akifuatiwa na Lando Noris nakupata ushindi wao wa kwanza tokea mwaka 2010 walivyoshinda Canadian Grand Prix.

Wakali hao wanatazamiwa kuchuana tena wikiendi ijayo kwenye mashindano ya Russian Grand Prix