Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 27Article 559768

Habari za michezo of Monday, 27 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Timu Zanzibar zakiri udhaifu kimataifa

Timu Zanzibar zakiri  udhaifu kimataifa Timu Zanzibar zakiri udhaifu kimataifa

KUKOSEKANA kwa mechi za kimataifa za majaribio na kutokuwa na ligi bora kumetajwa kuwa ni changamoto zinazofanya timu za Zanzibar kutolewa mapema katika michuano ya kimataifa.

Hayo yalisemwa na makocha wa timu za KMKM, Ame Msimu na wa Mafunzo, Said Kwimbi walipokuwa wakitoa tathmini zao juu ya ushiriki wa wa timu zao katika mashindano ya kimataifa na kutolewa mapema.

Kwimbi ambaye timu yake ya Mafunzo ilikuwa ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, alisema pamoja na kucheza mechi nyingi za kirafiki, lakini walihitaji mechi za majaribo za kimatiafa ili kupata uzoefu zaidi.

Alisema wachezaji wa timu yake ambayo ilitolewa na GD Inter Clube ya Angola hawakuwa na uzoefu kutokana na kukosa mechi za kirafiki za kimataifa.

“Kwa kweli niwe muwazi tu maana kukosekana kwa mechi za majaribio za kimataifa kumechangia kwa kiasi kikubwa kwa timu zetu kushindwa kuvuka hata hatua moja ya michuano tuliyoshiriki,” alisema.

Alisema walicheza mechi nyingi za kirafiki na timu za hapa nyumbani ambazo hazikuwasaidia kupata uzoefu wa kimataifa.

Hata hivyo, alisema kama timu zao zitajipanga vizuri zinaweza kufika mbali kwani mashindano hayo sio magumu sana.

Hata hivyo alisema wamejifunza kama unapokuwa nyumbani unatakiwa kutumia mbinu zako zote na kwamba mashindano hayo kwa yeye ameyaona ni sawa na vita vilivyokosa silaha.

Naye kocha wa KMKM iliyoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, Msimu alisema kikubwa kilichowaangusha ni ligi ya Zanzibar kutokuwa na ubora.

Alisema ligi hiyo haina ushindani mkubwa kiasi ambacho walikwenda kushiriki mashindano hayo wakiwa nyuma sana.

“Ligi yetu sio bora na inakosa ushindani na hii ndio sababu kubwa ya sisi kufanya vibaya, ila nizipongeze timu za Tanzania Bara kwa kuendelea kusonga mbele katika mashindano hayo,” alisema.

Katika michuano hiyo ya kimataifa, timu zote za Zanzibar zilitolewa baada ya Mafunzo kufungwa jumla ya mabao 4-0, ambapo nyumbani ilifungwa 1-0 na ugenini 3-0, huku KMKM wakifungwa jumla ya mabao 2-0.