Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 05 28Article 540394

Habari za michezo of Friday, 28 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Uchaguzi Mkuu wa TFF Agosti 7

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utafanyika Agosti 7, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema maamuzi hayo yalifikiwa kwenye kikao cha kawaida cha Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo kilichofanyika jijini.

Alisema kikao hicho pia kilijadili maendeleo ya mpira pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji na kujadili maendeleo ya miradi ya vituo vya soka vinavyojengwa Kigamboni na Tanga.

“Moja ya ajenda zetu ilikuwa ni uchaguzi mkuu, ni vizuri tunavyowasiliana kwa maandishi na mwenyekiti (wa Kamati ya Uchaguzi) ili naye aendelee na taratibu zake,” alisema.

Karia alisema pia katika kikao hicho walipokea taarifa kutoka Kamati ya Sheria ya shirikisho hilo kuhusu marekebisho ya baadhi ya kanuni za uendeshaji zinazosimamia kamati mbalimbali ikiwamo ya ukaguzi.

Uchaguzi Mkuu wa TFF hufanyika kila baada ya miaka minne. Mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2017 jijini Dodoma ambapo Karia aliingia marakani kwenye nafasi hiyo kwa mara ya kwanza, huku makamu wake akiwa, Michael Wambura.

Hata hivyo, Wambura hakumaliza miaka minne baada ya kuandamwa na kashfa ya ubadhirifu na kushitakiwa mahakamani.

Kwa sasa Katiba ya TFF imebadilishwa, hivyo makamu hatagombea tena bali Rais atapendekeza jina lake na kupigiwa kura kwenye mkutano mkuu.

Kwa sasa, Athumani Nyamlani ndio Makamu wa Rais aliyethibitishwa kwenye mkutano mkuu wa Desemba, 2019.

Kwa mujibu wa katiba ya sasa, kutakuwa na Makamu wa Pili wa Rais, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi.

Habari

Biashara

Burudani

Afrika

Maoni