Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 17Article 558073

Soccer News of Friday, 17 September 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Uchaguzi wa kikosi Simba pasua kichwa, Bocco nae yuko fiti

Simba SC wakijifua Jijini Arusha Simba SC wakijifua Jijini Arusha

Simba imewaambia mashabiki wake kwamba wachezaji wote wapo kamili na kilichobaki ni wao waje uwanjani wajionee Jumapili.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu ameliambia Mwanaspoti kuwa wachezaji wote wapo kamili haswa baada ya kucheza mechi tano za kirafiki kwa mafanikio makubwa na sasa wako tayari kuwavaa TP Mazembe kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Wachezaji wote 32 wako kwenye hali nzuri kwa hakika tunamshukuru Mungu, ninachoweza kuwaambia mashabiki wetu ni kuwa wajitokeze kwa wingi kuishuhudia timu yao,” amesema mwanachama huyo mwandamizi.

Alieleza kikosi kiko kwenye morali kubwa ya kuendeleza walipoishia kwani ndicho kitu muhimu ambacho wamekuwa wakikifanya ili kutimiza malengo ya timu waliyojiwekea.

“Msimu mpya kama unavyojua utakuwa mgumu kutokana na maandalizi ya kila timu lakini benchi la ufundi na wachezaji wetu wamejipanga kuhakikisha tunafanya kile tulichokifanya msimu uliopita kwa kutwaa mataji yote ambayo tunashiriki,” amesema.

MSIKIE HITIMANA

Kocha msaidizi wa kikosi hicho, Thierry Hitimana amesema kuongezeka kwake kwenye benchi la ufundi kunaipa wigo mpana timu hiyo na mbinu za kutamba popote.

“Umoja ni mshikamano na malengo yetu makuu ni kushinda kila taji msimu ujao, hivyo uwepo wangu, Matola na kocha wetu mkuu Gomes ni ishara tosha tunaelekea kwenye mstari ulionyooka,” amesema.

Matola amerejea kuungana na timu hiyo iliyoweka kambi Karatu mkoani Arusha baada ya kumaliza kozi yake ya ukocha aliyokuwa anasomea.

Ikiwa Morocco, Simba iliweka kambi katika mji wa Rabat na kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya FAR Rabat (2-2) na Olympique Club de Khouribga (1-1) na tangu irejee Bongo imecheza dhidi ya Coastal Union (0-0), ikashinda kwa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate na mchezo dhidi ya Aigle Noir ya Burundi wakashinda 2-1.

Baada ya mchezo huo kikosi cha Simba kilipaswa kucheza na Namungo FC lakini mchezo huo uliondolewa na sasa kinatarajiwa kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya kuwakabili TP Mazembe Jumapili.

BOCCO AONGEZA MZUKA KAMBINI

Nahodha wa Simba, John Bocco amerejea mazoezini kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi hicho kuelekea mechi ya Jumapili na ile ya Septemba 25, dhidi ya watani wao Yanga.

Bocco alikosekana huku taarifa zikidai kuwa alikuwa majeruhi hivyo kukosa mechi mbili za kufuzu Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na DR Congo na ile ya Madagascar.

Kwa upande wa TP Mazembe nao tayari wamerejea DR Congo kutoka Morocco walikokuwa wameweka kambi wakicheza mechi tatu za kirafiki.

Katika mechi tatu walizocheza Mazembe waliambulia ushindi kwenye mechi moja tu dhidi ya Club Chabab Riad Salim (1-0), sare moja dhidi ya Wydad Athletic Casablanca (0-0), na kupoteza moja kwa kufungwa mabao 2-1 na Sporting Club Chabab.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana kabla ya Jumapili ilikuwa ni Januari 31, ambapo zilitoka sare ya 0-0, katika mashindano maalumu yaliyoandaliwa na Simba yakifahamika kama Simba Super Cup.