Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 11 18Article 572437

Soccer News of Thursday, 18 November 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ulimboka: Simba, Ruvu lolote litatokea

Ruvu vs Simba Ruvu vs Simba

Si rahisi kihivyo! Ndiyo kauli ya mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe aliyetahadharisha mchezo wa keshokutwa wa Ruvu Shooting dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, siyo mwepesi na lolote linaweza kutokea.

Ulimboka amesema kuwa mchezo huo utakuwa muhimu kwa kocha mpya wa Simba, Pablo Franco kuangalia kwa upana kikosi chake na kumpa uelekeo mzuri wa vitu gani vya kuanza navyo na nini cha kuongeza.

Kocha huyo wa zamani wa Pamba alisema ni mchezo mgumu kwani Simba wanahitaji ushindi wa lazima lakini wanakutana na timu ambayo ina kocha mzuri na kikosi bora chenye bidii kinachopaswa kuheshimiwa, huku akieleza ugumu ama wepesi wa mchezo huo utategemea Ruvu wataingia na mipango ipi.

“Mchezo utakuwa mzuri lakini mgumu, Ruvu ni kipimo kizuri, wanacheza mpira mzuri ni timu ya kuiheshimu, lakini kocha wa Simba atautumia kuangalia kikosi kwenye ufanisi mkubwa kumpa uelekeo mzuri nini cha kuanza nacho na kuongezea,” alisema Mwakingwe na kuongeza.

“Uhitaji wa matokeo kwa Simba utategemea Ruvu wanaingiaje, chochote kinaweza kutokea, mashabiki wasiende na matokeo uwanjani, hata kama watapoteza nadhani kocha anahitaji pia kuona kama mambo anayoanza kuyaingiza kikosini yanafanya kazi,” amesema.

Mwenyekiti wa zamani Simba Mkoa wa Mwanza, Omary Makoye alisema; “Kocha anahitaji walau mechi tatu ama tano kujua uwezo wake kama ujio wake una tija, kikosi chetu tunakiamini mashabiki wasiwe na wasiwasi, tunapata alama tatu muhimu, tuna kazi moja tu ya kushinda”

Mwenyekiti wa Simba tawi la Isamilo jijini hapa, Salya Ludanha amesema;

“Kwa kweli tumejiandaa kwa vingi, kwanza ni ushindi, kuwapa hamasa wajiskie wako nyumbani, tunategemea makubwa zaidi hasa ukiangalia historia ya kocha tuna imani na tunategemea ujio wake utabadilisha mambo mengi,” amesema Ludanha.