Uko hapa: NyumbaniMichezo2022 01 15Article 585958

Soccer News of Saturday, 15 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Unaambiwa Simba ni Chama la Kibingwa

Unaambiwa Simba ni Chama la Kibingwa Unaambiwa Simba ni Chama la Kibingwa

EBANA Simba ni raha sana na kama unawachukua Simba kwa miaka ya hivi karibuni, basi ujiandae kununa sana. Simba juzi imeweka rekodi ya kufikisha kombe la nne la Mapinduzi huku Azam wakiendelea kuwa vinara baada ya kulitwaa kombe hilo mara tano. Hizi ndizo timu zilizotwaa kombe hili mara nyingi zaidi.

Bao la penalti iliyopigwa na Meddie Kagere dakika ya 56 lilitosha kabisa kuwapa Simba ubingwa wa nne wa Kombe la Mapinduzi mbele ya mgeni rasmi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ally Mwinyi.

Simba sasa imefikisha ubingwa mara nne wa Kombe la Mapinduzi na Azam FC inaendelea kuwa bingwa wa kihistoria kwa kulitwaa kombe hilo mara tano mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.

Kwa upande wa Simba, wameutwaa ubingwa huo mwaka 2008, 2011, 2015 na 2022. Yanga na Mtibwa ndizo zinafuata kwa kuutwaa ubingwa huo mara nyingi zikiwa zimeutwaa mwaka 2007 na 2021, na 2010 na 2020, mtawalia.

Timu pekee ya Zanzibar iliyowahi kuutwaa ubingwa huo ni Miembeni ambayo iliutwaa mwaka 2009, licha ya michuano hiyo kufanyika Zanzibar kila mwaka tangu ilipoanzishwa mwaka 2007.

Katika mchezo wa juzi, bao pekee la Simba lilitokana na penalti ya utata baada ya kipa wa Azam, Mathias Kigonya kumchezea faulo Pape Sakho ndani ya eneo la hatari, akiwa ameshaudaka mpira, akanyanyua mguu uliomgusa Sakho, na baada ya majadiliano ya muda mrefu, mwamuzi akaamua iwe ni faulo iliyochezwa katika eneo la hatari.

Azam walipinga faulo hiyo na ikapelekea mchezaji wa zamani wa Simba, Ibrahim Ajibu apewe kadi ya njano baada ya kumzonga mwamuzi akigomea maamuzi yake ‘simulation’.

Katika kipindi cha kwanza, Ajibu ambaye alicheza vizuri mechi hiyo, angeweza kuipatia Azam bao, lakini shuti lake kali la nje ya 18 liliokolewa na kipa Aishi Manula ‘Air Manula’ kwa juu na kwa ustadi mkubwa.

Simba nao walikosa nafasi kadhaa kupitia kwa Denis Kibu ambaye mashuti yake mawili kipindi cha kwanza yaliokolewa na Kigonya.

Simba sasa wanatarajiwa kurejea Dar kujiandaa na mchezo ujao ambao ni wa ligi dhidi ya Mbeya City utakaochezwa Jumatatu, Sokoine, Mbeya.