Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 04Article 541030

Habari za michezo ya

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Usajili wa Ambundo kama sio benchi, basi jukwaani

Usajili wa Ambundo kama sio benchi, basi jukwaani Usajili wa Ambundo kama sio benchi, basi jukwaani

TUFANYE zimebaki mechi nne tu Ligi Kuu Bara imalizike ingawa baadhi ya timu zimebakiwa na viporo hasa Simba na Namungo na zile timu wanazokutana nazo.

Wakati ligi inaelekea ukingoni, usajili unaanza kuvuma. Ule wa Ligi Kuu Bara, Daraja la Kwanza (FDL) na la Pili (SDL) na ligi zingine. Lakini kwa asilimia kubwa wadau wa soka waangalia usajili wa Ligi Kuu ambako kuna ushindani kuelekea msimu ujao. Ingawa kila timu inapambana kupata mafanikio kwenye zile nafasi nne za juu ambazo zitawapa nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa ya Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika - ile ambayo msimu huu imewakilishwa na Simba na Namungo FC.

Simba iliishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Namungo ilicheza Kombe la Shirikisho na kuishia hatua ya makundi. Nikirudi kwenye usajili, ni kwamba wakati kamati za usajili za klabu zikijadili mapendekezo ya makocha, basi wazingatie yatakayopendekezwa.

Inaeleweka timu shindani kwenye usajili, hasa Simba na Yanga ikiwemo Azam FC ambao hawana presha kubwa sana kwenye suala hilo, hupambana vilivyo kusajili.

Simba hadi sasa kikosi chao kinaeleweka ingawa watahitaji kufanya maboresho kidogo ukilinganisha na Yanga ambao wanaonekana kusuasua na wanahitaji usajili wa maana tu ili wawe na ushindani mkubwa.

Ndani ya timu hizo baadhi ya wachezaji wameanza kuongezewa mikataba na ukiona hivyo, basi ni wazi mchezaji huyo ana umuhimu mkubwa kwenye timu. Tumeona Simba na Azam wamefanya hivyo kwa nyota wao baadhi na wengine wanaendelea kufanya mazungumzo.

Upande wa Yanga wao bado, ila tumeona wakiachana na wachezaji akiwemo Carlinhos na wengine tukisikia kuwa wataachana nao.

Pia ndani ya timu hiyo kuna tetesi za kwamba wanamuwinda winga wa Dodoma Jiji, Dickson Ambundo anayemaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu.

Ni kweli yawezekana mchezaji huyo ni mzuri kwani hata kocha wa Simba, Didier Gomes alisifu kiwango chake, lakini je Yanga inamhitaji mchezaji huyo? (kama kweli) kwa ajili ya mafanikio ya haraka wanayoyataka ama kwa ajili ya kujenga timu?

Ambundo si mchezaji mbaya lakini anaweza kuwa mbaya kutokana na namna ambavyo Yanga ipo kwenye presha ya mafanikio makubwa japo kuifikia Simba kwa kiasi fulani ikiwemo kutwaa tu ubingwa wa ligi ama kombe la shirikisho. Yanga kama watamsajili mchezaji huyo basi wasiwe na haraka sana ya mafanikio, Ambundo awepo azoee presha ya Yanga ili baadaye awasaidie, maana imeonekana mara nyingi nyota wengi wanaosajili kwenye timu zenye presha basi si rahisi sana kuonyesha kile walichonacho na wanajikuta wamefeli badala ya kufanikiwa.

Lawama zinarudi kwao hasa pale mashabiki wanapohitaji makombe ama kuona timu yao inashinda kila mechi ama kila mashindano, hivyo usajili wa Ambundo kama atatua Yanga usije ukampa presha na kufeli kucheza, asajiliwe na wale wanaomsajili wajue kabisa kuwa yupo kwa ajili ya mafanikio ya baadaye.

Hata kama Simba nao watatamani Ambundo awe kwenye kikosi chao lakini anakwenda kucheza namba ya nani pale, bado atakuwa ni mchezaji wa kusikilizia benchi, atacheza lakini si kama anavyocheza sasa hapo Dodoma Jiji.

Wengi ndani ya Simba pia walifanya vizuri sana kwenye timu zao lakini walipofika hapo tunawaona kwenye benchi ama jukwaani kabisa, hata Ambundo lazima ataanzia kusugua benchi ama kushangilia jukwaani akiwaangalia wengine kwanza wanafanya nini ndani ya Simba.

Hivyo wasichukuliwe wachezaji kwa ajili ya kwenda kuonyesha jezi za timu zikiwa mwilini ama kuishia mazoezini lakini kucheza wasiwe na nafasi, wao watapata pesa nyingi lakini viwango vyao vinashuka kwa kasi ndani ya timu hizo.

Yanga wanapaswa kujitathimini zaidi wanakoelekea ili wasirudie makosa kwenye usajili wao, umakini na uchunguzi wa hali ya juu unapaswa kufanyika katika kuamua nani wa kumsajili, si kusajili ili mradi mchezaji ameng’aa katika mechi kadhaa tu, waangalie kiwango chake cha muda mrefu.

Natamani kuiona Yanga ile ya uwepo wa akina Thaban Kamusoko, Haruna Niyonzima (yule wa miaka ile sio wa sasa), Juma Abdul, Kelvin Yondani, Amissi Tambwe na wengine kibao.

Kikosi hicho naamini ingekuwa ndiyo miaka hii halafu ikakutana na Simba hii ya moto, hapo pasingetosha lakini kwa haraka haraka tu Yanga hii si ya ushindani mkubwa, lazima wafanye kitu cha maana msimu ujao na si kwa kusajili tu ili mradi wamesajili.

Tukutane dirisha kubwa la usajili ambalo limesogezwa mbele na tunasubiri kutangaziwa ni lini msako ramsi utaanza.

Join our Newsletter