Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 29Article 554260

Habari za michezo of Sunday, 29 August 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

WIKI YA MWANANCHI: Wameingia na kutoka Yanga SC

WIKI YA MWANANCHI: Wameingia na kutoka Yanga SC WIKI YA MWANANCHI: Wameingia na kutoka Yanga SC

WIKI inamalizika kwa namna yake hasa wale wapenda soka ambao ni wapenzi wa Yanga wakiwa na jambo lao pale kwa Mkapa watakapohitimisha ‘Wiki ya Mwananchi’.

Leo Yanga itatambulisha jeshi lake la mapambano kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na mashindano mbalimbali kuelekea msimu mpya wa 2021/22.

Tangu msimu uliopita wakati wakihitimisha ‘Wiki ya Mwananchi’ Agosti 30, 2020 timu hiyo imepita katika misukosuko mingi hasa kubadilisha makocha.

Kuelekea Wiki ya Mwananchi, Mwanaspoti linakuletea orodha ya makocha waliopita Jangwani kwa muda wa mwaka mmoja - yaani tangu Agosti 30, mwaka jana hadi sasa.

Zlatko Krmpotic

Alidumu Jangwani kwa siku 35 tu kisha safari ya kurudi kwao Yugoslavia iliwadia muda mfupi baada ya mchezo dhidi ya Coastal Union. Licha ya ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo huo, lakini haikubadili kitu.

Awali, alisaini mkataba Agosti 29 na kufukuzwa Oktoba 3, baada ya mchezo huo pale Uwanja wa Mkapa na nafasi yake kuchukuliwa na Cedric Kaze.

Kwa muda wa siku 35 alikuwa amekiongoza kikosi cha Yanga kwenye michezo mitano ya Ligi Kuu Bara akishinda minne na sare moja ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons - mchezo ambao ulikuwa wa kwanza kwao kwenye ligi pale Uwanja wa Mkapa, Septemba 6.

Cedric Kaze

Marchi 7, mwaka huu kibarua chake kiliota nyasi baada ya kutimuliwa pamoja na benchi nzima la ufundi akiwemo msaidizi wake, Nizar Khalifan; kocha wa makipa, Vladimir Niyonkuru na ofisa usalama wa timu, Mussa Mahundi.

Kaze alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuinoa Yanga, Oktoba 26, mwaka jana na aliiongoza timu hiyo katika michezo 18 ya Ligi Kuu akishinda 10, sare saba na kupoteza mmoja dhidi ya Coastal Union aliochapwa 2-1 Mkwakwani.

Yanga ilimtimua Kaze muda mfupi baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania Uwanja wa Sheikh Amri Abeid - Arusha na Juma Mwambusi kuchukua nafasi hiyo kwa muda.

Uamuzi wa mabosi wa Yanga ulikuja kutokana na matokeo mabovu waliyokuwa wakivuna hasa mzunguko wa pili wa ligi, ambapo katika michezo ya mzunguko huo ilikuwa inawaweka pabaya kubeba ubingwa.

Sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania ilikuwa mechi ya sita mzunguko wa pili wakiambulia pointi saba pekee wakidondosha alama 11 baada ya kushinda mechi moja, sare nne na kipigo moja.

Juma Mwambusi

Mwanzoni mwa mwaka jana alikiongoza kikosi hicho lakini aliondoka Januari 20 na Yanga ikatangaza nafasi yake kuchukuliwa na Nizar Khalfan aliyetangazwa Januari 27.Hata hivyo alirudi kivingine kama kocha mkuu wa muda wakati uongozi wa klabu hiyo ukisaka kocha wa kuziba nafasi ya Kaze baada ya kupoteza mwelekeo wa kubeba kombe la Ligi Kuu.

Nasreddine Nabi

Kocha huyu ataishuhudia kwa mara ya kwanza Wiki ya Mwananchi inavyokuwa na raha yake. Alianza kibarua hicho ndani ya Yanga Aprili 19, mwaka huu kwa Mtunisia huyo kukubali kumwaga wino.

Kabla ya Nabi ilielezwa uongozi wa Yanga ulishamalizana na Kocha Mfaransa Sebastian Migne, lakini akawa na masharti madogomadogo mengi kila mara jambo ambalo liliwashtua mabosi na kuachana naye.

Historia ya Nabi katika soka la Afrika inavutia kwani aliwahi kuifundisha Al-Ahli Benghazi (Libya) akidumu nayo kwa miezi minae kutoka Aprili hadi Desemba 2013.

Pia alizinoa klabu mbili kwa nyakati tofauti za Sudan akianza na Al-Hilal ambapo alidumu kwa miezi minne akiwa kocha mkuu kutoka Desemba 27, 2013 hadi Aprili 30, 2014 na mwaka huu aliiongoza Al -Merrikh katika hatua ya makundi alipochukua nafasi ya Didier Gomes Da Rosa ambaye kwa sasa yupo Simba.

Akiwa Misri aliifundisha Ismaily akidumu nayo kwa siku 22 kuanzia Januari 4 - 26 2016 na kule Italia aliinoa klabu ya daraja la tatu (Serie D), Pont Donnaz Hone Arnad akiwa kocha mkuu na kudumu nayo kwa miezi minne na siku 20 kutoka Julai 1 hadi Novemba 22, 2019.