Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 11 18Article 572590

Soccer News of Thursday, 18 November 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wakongwe wasema na Ajibu

Ibrahim Ajibu kuukosa mchezo dhidi ya Ruvu Shooting Ibrahim Ajibu kuukosa mchezo dhidi ya Ruvu Shooting

Wakati kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu akifunguka juu ya kuukosa mchezo wa kesho Ijumaa dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, nyota huyo ameonywa kuhusu kiwango chake.

Ajibu ameachwa kwenye msafara uliokwenda Mwanza kwenye mchezo huo wa raundi ya sita wa Ligi Kuu Bara kwa kile alichodai kuwa ni mgonjwa.

"Naumwa, ndio sababu sijasafiri na timu, ila zaidi kuhusu afya yangu muulize daktari, ingawa naendelea vizuri kiasi na nimekuwa nikifanya mazoezi binafsi kidogo kidogo baada ya wenzangu kuondoka," amesema Ajibu aliyewahi kuwa nahodha wa Yanga misimu mitatu iliyopita.

Daktari wa Simba, Yassin Gembe amesema Ajibu alipata majeraha madogo yaliyomsababishia maumivu ya kawaida.

"Ana maumivu madogo ambayo siku mbili au tatu hivi atakuwa ameimarika," amesema Dk Gembe.

Hata hivyo nyota wa zamani wa timu hiyo, Lubigisa Madata amemuonyoa Ajibu juu ya mwenendo wa kiwango chake.

"Anapaswa kutulia, ajitume na kuonyesha kiwango chake halisi," amesema Lubigisa na kuongeza.

"Hivi karibuni tumemuona, amepewa nafasi ya kucheza na ameonyesha kiwango kizuri sana ni kama amerudi kwenye ubora wake, tatizo lake ni moja tu, anaweza kucheza mechi mbili vizuri, halafu akapotea,"

"Aache masihara sasa, atulie acheze mpira, Ajibu ni mchezaji mwenye kiwango kikubwa mno kama ataamua kukitumia ipasavyo hata leo hii asingekuwa hapa nchini, angekuwa mbali zaidi."

Amesema kwa namna alivyomshuhudia Ajibu baada ya kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Simba hivi karibuni, amerudi kwenye kiwango, anastahili kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Pablo Franco.

"Akitulia na kujituma, Ajibu ana sifa zote za kuingia kwenye kikosi cha kwanza, tatizo lake ni moja tu, kujituma na kuendeleza ubora wake," amesema.   Hata hivyo Ajibu alipoulizwa juu ya maono hayo ya Lubigisa, na siri ya kiwango alichokionyesha baada ya kupata nafasi hivi karibuni, alicheka na kuomba aachwe.

"Hilo siwezi kulijibu kwa sasa," amesema Ajibu kwa kifupi jana huku akicheka.