Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 27Article 560014

Habari za michezo of Monday, 27 September 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Wanyama atundika daluga Kenya

Wanyama atundika daluga Kenya Wanyama atundika daluga Kenya

Baada ya kuitumikia timu ya taifa ya Kenya kwa miaka 14, kiungo Victor Wanyama anayecheza soka la kulipwa huko Canada katika timu ya Montreal leo ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu yake ya taifa 'Harambee Stars'.

Wanyama aliyeitumikia Harambee Stars kwa miaka 14 tangu Mei 27, 2007 alipoichezea kwa mara ya kwanza katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Nigeria waliopoteza kwa bao 1-0 amesema ameamua kupumzika ili kuwapa fursa nyota wanaoibuka kwenye soka kuitumikia Kenya.

"Wakati nakua ndoto yangu kila siku ilikuwa ni kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi yangu kwa fahari kubwa na ninaweza kusema ninaishi katika ndoto yangu.

Tangu nilipocheza mechi yangu ya kwanza dhidi ya Nigeria, miaka 14 iliyopita hadi kuwa nahodha wa timu katika Fainali za Mataifa ya Afrika huko Misri, miaka hii 14 imekwenda zaidi ya kile ambacho sikudhani kama kinawezekana

Tumeshirikiana nyakati kubwa kwa pamoja na ninaona fahari kuwa nahodha na kiongozi wenu," alisema Wanyama.

Wanyama alisema kwa sasa ndoto zake ni kuipa msaada Kenya nje ya uwanja

"Lakini siku zote mambo mazuri yanakuwa na mwisho na baada ya kujitafakari kwa muda mrefu nimeamua kuchukua uamuzi mgumu wa kustaafu soka la kimataifa.

Muda umefika kwangu kuachia timu kwa kizazi kijacho ili nao waweze kuweka alama na kusaidia timu ya taifa kwa mafanikio zaidi. Nategemea kurejea siku moja kusaidia shirikisho nje ya uwanja lakini kabla ya hapo nitaendelea kuwa shabiki mkubwa wa Harambee Stars na nitawashangilia nikiwa pembeni. Nashukuru kwa sapoti yenu," aliandika Wanyama katika taarifa yake ya kujiuzulu

Wanyama amestaafu kuitumikia Kenya akiwa ameichezea jumla ya mechi 64 na kuifungia mabao saba.

Kabla ya kujiunga na Montreal, Wanyama mwenye umri wa miaka 30 alizichezea timu za Nairobi City Stars, AFC Leopards, Helsingborg, Beerschot, Celtic, Southampton na Tottenham Hotspurs.