Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 18Article 552154

Soccer News of Wednesday, 18 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Waziri azitahadharisha Simba, Yanga 

Wawakilishi wa Tanzania Ligi ya Mabingwa Afrika Wawakilishi wa Tanzania Ligi ya Mabingwa Afrika

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amezipa tahadhari timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa na kuzitaka zisibweteke kwani hakuna timu ndogo kwenye mashindano.

Tanzania imetoa timu nne msimu huu kwenye michuano ya kimataifa ya CAF, ambapo Simba na Yanga zitashiriki Ligi ya Mabingwa na Azam na Biashara zitashiriki Kombe la Shirikisho.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa timu hizo kimataifa, Bashungwa alisema anazitakia kila la kheri katika maandalizi yao na kuzitahadharisha kuwa katika mashindano hakuna timu ndogo bali zijipange.

“Nawapongeza wote wanne kwa kuwakilisha taifa katika michuano ya kimataifa, niwape changamoto kwamba wasibweteke na kuwadharau wapinzani kwani hakuna timu ndogo katika mashindano, zijipange,” amesema.

Kwa mujibu wa droo iliyochezeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Simba itaanzia mzunguko wa kwanza huku timu nyingine za Tanzania zikianzia hatua ya awali.

Yanga itacheza na Rivers United ya Nigeria, Azam na Biashara zimepangwa kukutana na Horseed ya Somalia na FC Dikhil ya Djibouti.

Mechi za awali zitachezwa kati ya Septemba 10-12 kwa mkondo wa kwanza na zile za marudiano zitapigwa wiki moja baadaye na mshindi atafuzu raundi ya kwanza iliyopo Simba na vigogo wengine.

Simba katika mzunguko wa kwanza itasubiri mshindi wa mchezo kati ya Jwaneng Galaxy ya Botswana na DFC Beme ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Timu zote hizo ziko kwenye maandalizi ya michuano hiyo, Simba na Yanga zimeweka kambi Morocco, Azam FC ikitarajiwa kwenda Zambia na Biashara ikiendelea kujifua nyumbani kwake Mara.

Mbali na michuano hiyo ya kimataifa, Bashungwa amesema msimu ujao huenda ukawa mgumu hasa baada ya Ligi Kuu kupata udhamini mnono wa Azam Media wa Sh bilioni 225.

Amesema anachokiona hakutakuwa na timu ndogo wala kubwa hivyo vigogo waliozoeleka kutawala huenda wakakutana na upinzani mkali kama tu hazitajipanga vizuri.