Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 17Article 543214

Habari za michezo of Thursday, 17 June 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Yanga, Ruvu shoo shoo tu

Yanga, Ruvu shoo shoo tu Yanga, Ruvu shoo shoo tu

ACHANA na tambo zinazoendelea mitandaoni kutoka kwa timu zote, usiku wa leo kuna dakika 90 za shoo shoo zinazoshikilia hatma ya Yanga na Ruvu Shooting Jijini Dar es Salaam.

Ushindi kwa kila timu katika mechi hiyo itakayopigwa saa 1:00 usiku, ndio pekee unaohitajika ili kila upande ujiweke katika nafasi nzuri ya kubaki katika harakati za kutimiza malengo yake msimu na kinyume na hapo, matokeo ya sare ama kupoteza yatavuruga hesabu kwa kila timu.

Yanga inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi na pointi zake 61, hii ni fursa nzuri na muhimu kwao kuweka hai matumaini yao ya kutwaa ubingwa ikiwa wataibuka na ushindi katika mchezo wa leo na kuendelea kuwakimbiza Simba walio kileleni na pointi zao 67.

Kama Yanga itapoteza maana yake itarahisisha mbio za ubingwa kwa watani wao, kwani Simba itakuwa inahitaji pointi saba tu ili kutangaza ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo kwani Yanga hata ikishinda mechi zao nne zijazo itafikisa alama 73 tu.

Kocha msaidizi wa Yanga, Razack Siwa alisema; “Kuhusu suala la ubingwa bado ligi haijaisha na tumejipanga kuhakikisha tunashinda mechi zetu na mwishoni tutaangalia tumepata nini.”

Kwa upande wa Ruvu Shooting, leo wanalazimika kuibuka na ushindi, kwanza ili wajiweke katika nafasi nzuri ya kubakia katika Ligi Kuu msimu ujao lakini pia kuweka hai matumaini yao ya kumaliza katika nafasi nne za juu.

Pamoja na kuwa nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi na pointi zao 37, Ruvu Shooting bado hawako salama kwani utofauti wa pointi baina yao na timu mbili zilizo kundi la timu nne za mwisho ni pointi nne.

Ikiwa Maafande hao wataibuka na ushindi, wataweka hai matumaini yao ya kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ambayo inaweza kuwapatia fursa ya kushiriki mashindano ya klabu Afrika msimu ujao.

Wenyeji Ruvu wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa na mwenendo mbovu katika siku za hivi karibuni na kuthibitisha hilo, wamepoteza mechi nne mfululizo za Ligi Kuu zilizopita dhidi ya timu za Prisons, Mbeya City, Kagera Sugar na Simba.

Ni tofauti kidogo na Yanga ambayo katika mechi zake tano zilizopita, imeibuka na ushindi mara tatu, kutoka sare moja na kupoteza mchezo mmoja.

Yanga imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Ruvu Shooting ambapo imekuwa ikipata matokeo mazuri mara nyingi pindi wanapokutana nayo tofauti na Maafande hao ambao wamekuwa wakisota mbele yao.

Katika mechi 10 zilizopita baina ya timu hizo, Yanga imeibuka na ushindi mara nane, Ruvu Shooting wamepata ushindi mara moja na wametoka sare mara moja.

Mapema Mwadui na Mtibwa Sugar watavaana mjini Shinyanga odoma Jiji na KMC katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma. Simba inapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa msimu huu kutokana na takwimu zao na viporo walivyonavyo mkononi.