Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 05 27Article 540133

xxxxxxxxxxx of Thursday, 27 May 2021

Chanzo: globalpublishers.co.tz

Yanga: Tutapambana Mpaka Tone la Mwisho

BAADA ya timu yao kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la FA, Kocha wa Makipa wa Yanga, Razack Siwa, amesema wataendelea kupambana hadi dakika ya mwisho katika mashindano hayo na hatimaye kutimiza ndoto yao ya kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa msimu ujao.

Yanga imetoa kauli hiyo baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mwadui FC na sasa itakutana na Biashara United katika hatua inayofuata.

Akizungumza na gazeti hili, Siwa alisema wao wataendelea kujiimarisha ili kupata matokeo bora na kamwe hawatajali au kuangalia matokeo ya timu nyingine.

Siwa ambaye ni raia wa Kenya, alisema wamefurahishwa na ushindi na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wao kwa sababu wamefikia malengo yaliyokusudiwa.

“Tumecheza vizuri na kupata ushindi. Ushindi ni ushindi tu, uwe wa goli moja, mawili ni ushindi na kwa haya tunayoyapata sasa matumaini yapo. Tutapambana hadi dakika ya mwisho bila kuangalia timu nyingine inafanya nini. Sisi tunaendelea na mapambano na mwisho wa michezo ndipo kila kitu kitaamua,” alisema Siwa.

Aliongeza mechi zote zilizobakia za Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano hiyo ambayo bingwa wake ataiwakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo wataendelea kujiimarisha zaidi.

Naye Kocha wa Mwadui FC, Salhina Mjengwa, alisema timu yake ambayo msimu ujao itashiriki Ligi Daraja la Kwanza imepoteza mechi hiyo kutokana na makosa binafsi yaliyofanywa na baadhi ya wachezaji wake.

Mjengwa alisema kuna baadhi ya vitu ambavyo wachezaji wake walifanya havikuwa na ulazima walitaka kuvizidisha, ndiyo maana wamepoteza mechi hiyo.

“Goli la kwanza lilikuwa kosa la golikipa na hata goli la pili haikuwa na sababu yoyote ya mchezaji kutaka kupiga chenga pale, kapokonywa ikapigwa ndefu tukafungwa,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro.

Aliwapongeza Yanga kwa kutumia makosa ya wachezaji wake na kupata ushindi uliowapeleka hatua inayofuata na kuongeza kwa sasa wanakwenda kujipanga upya kwa ajili ya kushiriki na Ligi Daraja la Kwanza.

“Tumeshuka daraja, tumetolewa katika robo fainali, sasa tunakwenda kufanya maandalizi ya kushiriki Ligi Daraja la Kwanza,” alisema Mjengwa.

Simba ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo na jana usiku ilishuka dimbani kuvaana na Dodoma Jiji FC kutoka Dodoma katika mechi ya robo fainali ya mwisho iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo…Azam FC imefanikiwa kusonga mbele katika michuano hiyo baada ya kuifunga Rhino Rangers mabao… katika mechi ya robo fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga. Azam sasa itacheza hatua ya nusu fainali dhidi ya mshindi wa mechi kati ya Simba na Dodoma Jijini.

Join our Newsletter