Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 17Article 558082

Soccer News of Friday, 17 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Yanga kutangaza vivutio vya Utalii Kimataifa

Jezi za Yanga zinazotangaza vivutio vya Utalii zikitambulishwa mbele ya Wanahabari Jezi za Yanga zinazotangaza vivutio vya Utalii zikitambulishwa mbele ya Wanahabari

Klabu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga), imeingia makubaliano na Wizara ya Maliasili na Utalii, ya kuvaa jezi zenye nembo ya VISIT KILIMANJARO & ZANZIBAR kwenye michezo yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ambayo Septemba 19, itakuwa uwanjani kule nchini Nigeria kukipiga na Rivers United ya nchini humo kwenye mechi ya mkondo wa pili hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza Kaimu Mtendaji mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa, amesema wao kama sehemu ya Taifa wanajitolea bure bila malipo yoyote kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wanalitangaza Taifa.

"Kama mnavyofahamu sisi ni timu ya wananchi, pamoja na kushiriki katika michezo, lakini tuna wajibu pia wa kuungana na Serikali katika mambo makubwa yenye faida kwa watanzania wote"

"Tunaungana na Bodi ya Utalii kupitia Wizara ya Mali Asili na Utalii kwa ajili ya kutanzaza utalii wetu kimataifa" amesema Mfikirwa.

"Mnafahamu Yanga inashiriki Mashindano ya Kimataifa hivyo tutachangia kutangaza Utalii na kwa kuanza tumeanza kuutangaza Mlima Kilimanjaro na Zanzibar"

"Kwenye jezi zetu sehemu ambayo yanakaa matangazo sisi tumeamua kuweka hiyo nembo kama sehemu ya kujitolea kwa Serikali ambayo inafanya juhudi kubwa kuutangaza Utalii, na pengine mbeleni tutakuja na wazo bora zaidi"

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii nchi Jaji Mstaafu Thomas Mihayo nae amewashukuru na kuwapongeza Yanga kwa kukubali kushirikiana na Bodi yake kutangaza Utalii wa Tanzania.

"Nawashukuru sana klabu ya wananchi kuungana nasi kutangaza Utalii wa Tanzania, kwa Klabu kama Yanga kukubali kutangaza Utalii wetu bila kulipwa ni mchango mkubwa sana na nwashukuru sana kwa uzalendo wao"

"tunawaombea huko wanapokwenda wakashinde ili waendelee kuitangaza Tanzania popote pale wanapokwenda, hilo lazima tuwasifie maana utalii unaingiza fedha nyingi sana za kigeni" amesema Jaji Mstaafu Mihayo.

Nae waziri wa Mali asili na Utalii Damas Ndumbaro, alikuwa na machache ya kuzungumza;

"Tunawashukuru Yanga kwa wazo lao la kujitolea bure kabisa kutangaza utalii kupitia michezo, leo Yanga imekua timu ya kwanza Tanzania kuunga mkono kwa vitendo 'Royal Tour' ambayo Rais ameifanya".

"Kwa hiyo niwaeleze kabisa Serikali ipo na nyinyi na tunathamini hiki ambacho mmekionesha leo na wengine bila shaka wataiga na kufuata kutoka kwenu". amesema Ndumbaro