Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 09 08Article 556066

Soccer News of Wednesday, 8 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Yanga kutest mitambo ikiisubiri Rivers Utd

Afisa Habari wa Klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli Afisa Habari wa Klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli

Klabu ya Yanga inajiandaa na mchezo dhidi ya Rivers United ya Nigeria Septemba 12 ikiwa ni mchezo wa hatua ya awali kufuzu makundi ya Ligi ya mabingwa barani Afrika katika Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Yanga, ambayo imeshajitupa dimbani mara nne hadi sasa, ambazo ni dhidi ya Zanaco ya Zambia katika kilele cha wiki ya Mwananchi, DTB, Friend Rangers na Pan Africans, imeeleza kuwa inatarajia kupata mchezo mwingine mmoja kabla ya kuwavaa Wanaigeria hao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, amesema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi, ameuagiza uongozi kukitafutia kikosi chake mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya Jumapili.

“Kocha amesema wiki hii tutakuwa na mchezo wa mwisho wa kirafiki, ambao utatupa picha halisi kuelekea katika mchezo wetu wa kimataifa,”amesema Bumbuli.

Bumbuli amesema timu hiyo inaendelea vizuri na mazoezi na kila mchezaji akiwa na morali ya kufanya vizuri katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa, ambao wataanzia nyumbani.

Wakati huo huo, Msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara, amesema kutinga hatua ya makundi ndiyo lengo mama na baada ya hapo wataangalia kinachofuata mbele.

"Tunajiandaa ndani na nje ya uwanja. Ndani ikiwa na maana ya uwanjani na nje ikiwa na maana kuutangaza na kuhamasisha mashabiki wajazane uwanjani kuipa sapoti timu yetu, lengo letu la kwanza msimu huu ni kutinga hatua ya makundi. Baada ya hapo tutaangalia nini kinaendelea mbele, lakini kwanza kabisa makundi." amesisitiza manara

Kuhusu maandalizi ya mchezo huo, amesema yanaendelea vvema na wanachotaka kufanya Jumapili si kupata ushindi tu, bali ushindi mnono, ambao utawaweka vizuri kuelekea kwenye mechi ya marudiano nchini Nigeria.

"Lengo si kupata ushindi tu, ila ushindi mnono ili kujiweka vema na mechi ya marudiano. Nimeona watu wanauliza kama mechi itakuwa na watu au watazuiwa kama ilivyokuwa kwenye mechi ya Taifa Stars na Madagascar, lakini ninavyojua ni kwamba mechi za kufuzu Kombe la Dunia zinasimamiwa na FIFA ambao wanazuia mashabiki, ila za Ligi ya Mabingwa zinasimamiwa na CAF. Nadhani wao hata kama watazuia, lakini wataruhusu idadi fulani ya mashabiki kuingia," amefafanua Manara