Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 07 13Article 546835

Soccer News of Tuesday, 13 July 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Yanga sasa kambi ni Ulaya

Yanga sasa kambi ni Ulaya Yanga sasa kambi ni Ulaya

MASHABIKI wa Yanga wana kila sababu ya kutembea kifua mbele mtaani, kwani kwa sasa chama lao, linapitia wiki ya jeuri ya fedha na vurugu zao zinawatingisha mpaka watani wao Simba na siri kubwa imefichuka kumbe ni bilionea wao, Ghalib Said Mohammed ambaye ndani ya wiki chache amefanya mambo mazito.

Mashabiki wa Yanga wanashangilia bado shangwe la ushindi wa bao 1-0, lakini mtaani wanaringa na dili la mabilioni la Azam Media na sasa kuna mazito mengine yamefanyika kutoka kwa Ghalib ambaye anamiliki kampuni ya GSM inayoidhamini na kuifadhili Yanga.

PATI NZITO YA SH500 Milioni

Ghalib juzi aliwaandalia pati moja ya maana wachezaji wake na makocha wao na ndani pia wakaalikwa vigogo kibao wakisherehekea ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba ambao ulichelewesha sherehe za ubingwa za Wekundu wa Msimbazi.

Katika tafrija hiyo, Ghalib alitimiza ahadi yake kibabe akiwakabidhi vijana wake mkwanja wa maana Sh500 milioni alizowaahidi endapo wataifunga Simba na baada ya hapo akawaambia kazi kwenu wapigeni tena Julai 25 pale Kigoma kuna nyingine zaidi ya hizi.

Yanga itakutana na Simba Julai 25 katika Fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) utakaopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani humo ukiwa ni mchezo wa nne ndani ya msimu mmoja, baada ya ile ya fainali ya Kombe la Mapinduzi 2021 na mbili za Ligi Kuu Bara.

BASI LA ULAYA LATUA JANGWANI

Akiwa bado hajapoa Ghalib amelishusha basi la kisasa kutoka kampuni ya Scania maalum kwa timu hiyo ambalo ni kama amerusha kombora jingine kwa Simba akijibu mapigo ya basi la wekundu hao.

Simba wiki chache zilizopita walitambulisha basi lao la kisasa kutoka kampuni ya TATA ambalo walinunuliwa na bilionea wao Mohamed ‘Mo’ Dewji.

Yanga wameshashusha lao aina ya Scania Aris, ambalo ukiangalia Ulaya ni kama lile linalotumiwa na klabu kubwa za Real Madrid na Liverpool ambalo hata kama utalipata si kwa chini ya Sh 700 milioni.

Basi hilo Mwanaspoti linafahamu linafanyiwa kazi ya kuwekwa karatasi maalum za klabu hiyo na kwamba Ghalib anataka litambulishwe rasmi kesho Julai 13.

USAJILI WA KISHINDO

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Athuman Kihamia amefichua ukiachana na vurugu hizo lakini hatua kubwa ya Ghalib ni kwamba anakuja kufanya usajili wa kishindo kuelekea msimu ujao.

Kihamia ambaye pia ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa ndani ya wanachama, ameliambia Mwanaspoti kwamba bilionea huyo atashusha mastraika wawili, beki na kiungo ikiwa ni harakati za kusuka kikosi chao ili timu itishe uwanjani.

“Watu wasidhani huyu Ghalib amekuja kujaribu Yanga, amedhamiria kweli, akiahidi huwa anatekeleza bila wasiwasi na subirini kishindo cha usajili, kuna mastraika wakubwa wenye rekodi wanakuja hapa Yanga siku sio nyingi,” alisema Kihamia ambaye ni mteule wa Rais akiwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha na kuongeza;

“Hilo basi sio kwamba ni basi la kawaida kama ambayo tumewahi kuyaona yanatambulishwa hapa nchini, nafikiri wanachama wetu na mashabiki wazidi kutulia na kuwa wamoja ili waone nguvu zaidi ya huyu mtu.”

Aidha, Kihamia aliongeza hata mkataba wa Azam Media ambao Yanga inaushangilia una msukumo mkubwa wa Ghalib.

“Leo Yanga wanashangilia mkataba huu wa Azam Media, lakini mimi najua kwamba aliyefanya mazungumzo haya na viongozi wa juu wa Azam Media ni Ghalib na hatimaye sasa tutapata nguvu hii ya fedha,” alisema Kihamia na kuongeza;

“Akili yake ni tofauti angeweza kutaka kuona hakuna fedha zinazoingia ili aonekane nguvu yake lakini nimekuwa nikiongea naye na kiu yake ni kutamani kuona Yanga inakuwa na vyanzo vingi vya kuingiza fedha ili timu ijiendeshe.”

KAMBI SASA ULAYA

Kama ratiba zitaenda sawa Mwanaspoti linafahamu kwamba kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi ameambiwa achague wapi anataka kwenda na timu yake kwa maandalizi ya msimu na kwamba uko mpango wa kuipeleka timu hiyo nchini Uturuki kwa kambi hiyo.

Hapa Ghalib kama hesabu hizi zitakwenda sawa atakuwa anarudisha ufalme wa Yusuf Manji ambaye aliwahi kuipeleka timu hiyo nchini humo kwa nyakati mbili tofauti.