Uko hapa: NyumbaniMichezo2022 01 08Article 584080

Soccer News of Saturday, 8 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Yanga v Azam, Simba v Namungo Nusu Fainali Mapinduzi

Yanga v Azam, Simba v Namungo Nusu Fainali Mapinduzi Yanga v Azam, Simba v Namungo Nusu Fainali Mapinduzi

KITU pekee ambacho mashabiki wa Simba na Yanga wanakifurahia kwa sasa ni kuziona timu hizo zikiendelea kukipiga kwenye Kombe la Mapinduzi licha ya kubanwa kwenye mechi zao za mwisho za makundi.

Vigogo hao wa soka bara licha ya kuwa na sehemu kubwa ya vikosi vyao lakini walishindwa kuzibeba pointi tatu kwenye mechi hizo za mwisho ambapo waliambulia pointi moja tu.

Yanga ndiyo walikuwa wa kwanza kucheza ambapo walitoshana nguvu na KMKM kwa kufungana mabao 2-2 kisha Simba wao wakashindwa kuziona nyavu za Mlandege na kutoka nao suluhu.

Simba walicheza saa 2:15 usiku. Matokeo hayo yanazibeba timu hizo na kuzifanya zitinge hatua ya nusu fainali ambapo Yanga wanatarajiwa kuvaana na Azam FC huku Simba wakicheza na Namungo FC.

Kwa mujibu wa kanuni za Kombe la Mapinduzi zinamtaja kinara wa kundi B ambalo Yanga wamemaliza wakiwazidi KMKM mabao ya kufunga kukutana na kinara wa Kundi A ambapo hadi sasa Azam wanakamata nafasi ya kwanza wakiwa na pointi sita huku wakitarajiwa kumaliza mechi yao ya makundi leo Jumamosi dhidi ya Yosso Boys.

Kanuni hizo pia zinabainisha kuwa kinara wa kundi C ambalo Simba walimaliza wakiwa kileleni kuvaana na mshindi wa pili wa kundi A ambao ni Namungo walishika nafasi hiyo baada ya kumaliza mechi zake tatu wakiwa na pointi sita.

Katika mchezo wa Yanga wenyewe walishindwa kuzilinda pointi tatu baada ya KMKM kusawazisha bao katika muda wa jioni na kuifanya mechi imalizike kwa sare ya mabao 2-2.

Mabao ya Yanga ambayo kwenye michuano hiyo inaongozwa na kocha Cedric Kaze yalifungwa na straika Heritier Makambo na Feisal Salum. Makambo ndiye kinara wa mabao katika kikosi hicho akiwa na mabao mawili.