Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 06 15Article 542731

Habari za michezo of Tuesday, 15 June 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Yanga yaipora Mazembe kiungo, ni fundi wa mpira

Yanga yaipora Mazembe kiungo, ni fundi wa mpira Yanga yaipora Mazembe kiungo, ni fundi wa mpira

YANGA inaendelea kuunda jeshi lake kwa hesabu kali na bado wameganda DR Congo na safari hii sasa wamemrudisha njiani kiungo mmoja fundi wa mpira aliyekuwa anaelekea kujiunga TP Mazembe inayopambana pia kuunda kikosi kipya.

Mabingwa hao wa zamani wa Afrika, wamekuwa na msimu mbaya kiasi cha kushindwa kutetea ndoo ya Ligi Kuu ya nchini kwao na pia kuchemsha katika Ligi ya Mabingwa Afrika iking’olewa hatua za makundi, lakini katika mipango yao ya kujisuka upya ikakutana na mziki wa Injinia Hersi Said.

Iko hivi. Kwenye faili la mabosi wa Yanga walikuwa na jina moja la kiungo Ciel Ebengo ambaye ni Mkongoman aliyeripotiwa na Mwanaspoti wiki iliyopita kuwa wamemfuata kumbeba akiwa anaitumikia klabu ya FC Lupopo lakini ghafla wakashtuka na kubadilia gia angani.

Mwanaspoti ilidokeza juu ya hesabu hizo za Yanga kwa Ebengo anayetumia mguu wa kushoto, lakini taarifa za uhakika imezipata ni kwamba safari ya injinia Hersi Said, Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM wanaoidhamini Yanga akisimamia pia kusajili wachezaji wa timu hiyo, alishtukia kitu kufuatia kikao cha kocha mmoja mkubwa nchini huyo aliyeanika udhaifu wa kiungo huyo.

Kutokana na kupenyezewa faili zima la Ebengo, Yanga iliamua kusitisha usajili wake na mtu aliyesababisha dili kutibuka ni kiungo mwingine Mercey Vumbi Ngimbi anayeichezea Union Maniema iliyomaliza nafasi ya tatu msimu huu.

Ngimbi alikuwa amekamilisha mazungumzo karibu kila kitu kusajiliwa na TP Mazembe kwa mkataba wa miaka mitano, lakini baada ya Yanga kupenyezewa wasifu wake na kutibuliwa kwa dili la Engo, naye aliamua kubadili gia angani na kukubali mkataba wa miaka miwili Jangwani.

Ngimbi aliona mkataba wa Mazembe ni mrefu, lakini pia uwepo wa kasumba la mabosi wa timu hiyo kutaka dau kubwa pale mastaa wake wanapopata timu nje, ambayo imekuwa ikiwakwaza wachezaji wengi wakubwa kujiunga nayo, ikamfanya naye abadili mawazo na kuitaka Yanga.

Taarifa za uhakika ni kwamba Hersi kwa sasa yuko hatua za mwisho kumalizana na klabu ya Maniema, iliyowauzia Yanga winga Tuisila Kisinda na beki wao ghali Shaban Djuma.

Hata hivyo, usajili huo wa Ngimbi pia atashukuriwa zaidi kiungo na nahodha msaidizi wa Yanga, Mukoko Tonombe aliyelainisha biashara hiyo akiwa Tunisia na kiungo huyo ndani ya timu ya taifa walipoenda kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa.

Ngimbi amerejea jana nchini Congo na tayari ameshawaambia mabosi wa Maniema kwamba waachane na dili la Mazembe anataka kwenda Yanga ya Tanzania ili aungane na Mukoko, Kisinda na Djuma ambapo sasa biashara imebaki Yanga kumalizana na uongozi wa Maniema.

NGIMBI HUYU HAPA

Jana mchana Ngimbi ambaye ni nahodha wa Maniema amelithibitishia Mwanaspoti kwa kusema; “Ilikuwa niende Mazembe kweli lakini sasa nimeona nikasajili Yanga nataka kuondoka hapa Congo sasa.”

Msimu huu ambao Maniema imemaliza nafasi ya tatu nyuma ya Mazembe, Ngimbi alifunga mabao saba na kutoa asisti 9 za mabao, kuonyesha ni mchezaji wa aina gani.

Usajili huo endapo utakamilika utamaanisha maisha ya kiungo mkongwe, Haruna Niyonzima ndani ya Yanga yatakuwa yametamatika baada ya mkataba wake kumalizika mwisho wa msimu huu.