Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 30Article 554281

Habari za michezo of Monday, 30 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

Yanga yasimamisha nchi kwa Mkapa

Yanga kusimamisha nchi kwa Mkapa Yanga kusimamisha nchi kwa Mkapa

Yanga inahitimisha Wiki ya Mwanachi baada ya shughuli mbalimbali za kijamii zilizofanyika kupitia wanachama, mashabiki na viongozi wa klabu hiyo kote nchini kwa muda wa wiki nzima, ambapo watalitumia tamasha hilo kutambulisha wachezaji wa msimu mpya kuelekea msimu wa 2021/22.

Mbali na utambulisho huo wa wachezaji, pia kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiongozwa na mwanamuzi nguli na mkongwe wa muziki wa dansi kutoka DRC Kongo, Koffi Olomide, ambaye alitua Uwanja wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana mchana na kupokewa na Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara sambamba na mashabiki wa timu hiyo.

Mbali na Koffi, Mkuu wa Idara ya Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli, alimwambia mwandishi wetu katika jukwaa la burudani watakaowapagawisha mashabiki kwa muziki ni pamoja na Shilole 'Shishi Baby', Chege Chigunda, Mh. Temba, Juma Nature a.k.a Kiroboto, Mzee wa Bwax na wengineo wengi.

Bumbuli alisema maandalizi yote yamekamilika na kuwataka Wananchi kuhudhuria kwa wingi ili kushuhudia utambulisho huo, lakini pia kupata burudani ambayo anaamini hakuna atakayejutia kiingilio chake.

"Maandalizi yoye yamekamilika na milango kesho (leo), itakuwa wazi kuanzia saa tatu asubuhi, hivyo wanachama na mashabiki wa Yanga, lakini na Watanzania wote kwa ujumla waje kwa wingi bila kukosa, kushuhudia tukio hili kubwa," alisema.

Aidha, alisema baada ya shughuli nzima ya utambulisho na burudani ya kukata na shoka kutoka kwa wasanii hao, mashabiki watashuhudia mechi kali dhidi ya Zanaco ya Zambia ambayo tayari imeshawasili Dar es Salaam tangu juzi.

Kuhusu wachezaji waliokuwa wamebaki nchini Morocco, Bumbuli alisema: "Wote wameshawasili na watakuwapo uwanjani kesho, hivyo mashabiki waje kwa wingi kuwashuhudia katika Kilele cha Mwananchi".

Katika mechi hiyo, pia mashabiki watapata fursa ya kushuhudia nyota wapya wa kikosi hicho wakiichezea timu yao kwa mara ya kwanza kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara utakaofunguliwa rasmi Septemba 25, mwaka huu kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Simba huku ligi hiyo ikianza siku nne baadaye.

Baada ya tamasha hilo, Yanga itarejea kambini Kigamboni kuendelea kujiandaa kwa mchezo mgumu wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria, utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kati ya Septemba 10-12, mwaka huu kabla ya kurudiana ugenini baada ya wiki mbili.