Uko hapa: NyumbaniMichezo2021 08 12Article 551182

Soccer News of Thursday, 12 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Yanga yawatuliza mashabiki kuuzwa Kisinda

Mahabiki wa Klabu ya Yanga Mahabiki wa Klabu ya Yanga

Uongozi wa klabu ya Yanga umewataka mashabiki wa timu hiyo kujivunia ubora wa kikosi chao, badala ya kuwalaumu kwa kumuuza Tuisila Kisinda kwenda klabu ya RS Berkane ya Morocco.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa klabu hiyo, Dominic Albinus aliwataka mashabiki wasiusakame uongozi wao kwa kumuuza mchezaji huyo, kwani msimu ujao kikosi chao kitakuwa imara zaidi baada ya kusajili wachezaji nyota.

Alisema wamesajili wachezaji wenye ubora wa aina yake kwa ajili ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.

“Unapokuwa klabu ambayo wachezaji bora wanakiri kushawishika kujiunga nawe, inadhihirishia daraja lako kuwa ni kubwa kiasi gani, ofa ya Kisinda kwenda RS Berkane inakuonesha Yanga ni klabu kubwa kwa kusajili wachezaji kutoka Congo, Mali na Uganda,” alisema Albinus.

Kiongozi huyo alikana madai kuwa Yanga inataka kuwauza wachezaji wake wote nyota, ambapo alisema lengo lao ni kuimarisha kikosi chao.

Alisema kikosi chao kiko tayari kwa ajili ya msimu ujao na kitaondoka nchini wiki ijayo kwenda Morocco kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kauli ya kiongozi hiyo inatokana na usajili ambao timu hiyo imeufanya kwenye kipindi hiki ambao umekusanya idadi kubwa ya wachezaji nyota walioainishwa kwenye ripoti ya kocha Nasreddine Nabi.

Alisema `wamevunja benki’ ili kusajili wachezaji nyota na wenye uwezo wa kurejesha heshima ya timu hiyo baada ya kukosa mataji misimu kadhaa.

“Ukweli Yanga tumedhamiria kurudisha heshima yetu ndio maana tumetumia gharama kubwa kukiboresha kikosi chetu lengo ni ubingwa wa ligi na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ambayo hatujashiriki kwa misimu miwili sasa,” alisema Abinus.

Kiongozi huyo alisema mpaka kufikia Jumamosi ijayo watakuwa wamekamilisha mchakato wote wa usajili na watakuwa katika maandalizi ya mwisho kujiandaa na safari ya Morocco kwa ajili ya kambi ya kujiandaa na msimu ujao.

Alisema baada ya kumtambulisha kipa Erick Johola wamebakisha nafasi mbili za wachezaji wa kigeni na mmoja ambaye ni beki wa kati Yannick Bangala tayari yupo nchini na wanatarajia kumtambulisha muda wowote baada ya kukamilisha mazungumzo ya kusaini mkataba wa kuitumikia timu yao.