Uko hapa: NyumbaniBurudaniMuziki2021 02 08Article 523732

xxxxxxxxxxx of Monday, 8 February 2021

Chanzo: habarileo.co.tz

Marioo, Dulla Makabila, Kassim Mganga waikamata Dodoma

WASANII 10 jana walitoa burudani ya kukata na shoka katika hoteli ya Royal Village Dodoma kuashiria ujio wa tamasha la Serengeti katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma jana.

Miongoni mwa waliohudhuria tamasha hilo lililopewa jina la Serengeti Royal Pre Party ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu Habari Dk Hassan Abbasi na viongozi wa Serikali na wabunge.

Msanii Marioo alitoa burudani ya kufa mtu na kibao chake cha Mama Amina na kuvuta hisia ya Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale ambaye alishindwa kuzuia na kwenda kumpongeza.

Tajiri wa mahaba Kassim Mganga akidondosha burudani iliyosheheni mahaba mazito kutoka kumbukumbu ya Awena, akifuatiwa na wasanii wengine kama Mr Blue, Nandy, Mfalme wa Singeli Dulla Makabila, Linnah na wengine wengi.

Shamra shamra za tamasha hilo zilitanguliwa na michezo miwili iliyochezwa katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ambapo timu za mashabiki wa timu za Simba na Yanga ambao ni madereva bodaboda na bajaji Dodoma walichuana.

Timu ya mashabiki wa Yanga waliibuka kidedea kwa kuwafunga mashabiki wa Simba kwa penalti 8-7 baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 kwa suluhu.

Mechi ya pili ilihusisha timu za wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao watatumbuiza katika tamasha hilo dhidi ya timu inayoundwa na viongozi wa serikali ya wanachuo kutoka vyuo vikuu vilivyopo mkoa wa Dodoma.

Timu ya wasanii ilishinda kwa penalti 3-2 na mlinda mlango wa timu ya wasanii Khalid Ramadhan ‘Tundaman’ alipangua penalti moja.

Join our Newsletter