Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 05 04Article 536284

Habari za Biashara of Tuesday, 4 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

ATCL kupasua anga China

ATCL kupasua anga China ATCL kupasua anga China

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) inatarajia kuanza safari kwenda mji wa Guangzhou nchini China wiki hii.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema jana Dar es Salaam kuwa, kuanza ka safari hizo ni matokeo ya kufikiwa makubaliano baina ya China na kampuni hiyo hasa kuhusu kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Matindi alisema ndege ya ATCL inatarajiwa kwenda China mara moja kila baada ya wiki mbili ikiwa na raia wa China na wengine wenye vibali maalumu vya kuishi nchini humo.

Alisema kwa safari za kurudi Tanzania abiria yeyote ataruhusiwa kuja na ndege hiyo.

“Hatua hii inatokana na uamuzi uliofikiwa na nchi hiyo kwa kuzuia vibali kwa watu wengine wasio raia wao kuingia nchini wakilenga kujikinga na ugonjwa huo, lakini kadri tunavyoendelea imani yetu mambo yatabadilika na kuruhusu abiria wote kusafiri,” alisema Matindi.

Aidha, alisema ili abiria asafiri na ndege hiyo itakayotumia wastani wa saa 14 kutoka Dar es Salaam hadi China, atalazimika kufanyiwa vipimo vitatu vya Covid-19 siku tatu mfululizo kabla ya safari na pia siku ya safari atapimwa kipimo kingine cha haraka.

Alisema suala hilo lilikuwa changamoto iliyosababisha kuchelewa kuanza kwa safari za kwenda China kwa kuwa Serikali ya China ilipendekeza kipimo cha Covid-19 cha ‘IGM’ kinachotumika nchini humo na kupendekeza abiria wanaotaka kusafiri kutoka Tanzania wafanyiwe kipimo hicho ndipo wapewe vibali vya kusafiri.

“Tunaishukuru serikali yetu iliwezesha kupatikana kwa kipimo hicho cha IGM ambapo pamoja na kipimo kijulikanacho kama PCR, itamlazimu kila msafiri kufanyiwa ili kujiridhisha kama hana corona ndipo aweze kusafiri,” alisema mtendaji huyo wa ATCL.

Alisema wanatarajia kuwa ndege hiyo itakuwa ikifanya safari kila Jumamosi kuanzia saa 11 alfajiri na itafika China saa 3 usiku na kisha itaondoka saa 5 usiku huo kurudi Tanzania inatarajiwa kuwasili Jumapili saa 5 asubuhi.

Alisema kwa wasafiri wanaotarajiwa kusafiri kwa ATCL kwenda China watalazimika kukata tiketi ya safari hiyo kupitia mawakala watatu na kwamba, majina ya mawakala hao yanapatikana katika tovuti ya shirika hilo.

Matindi alisema safari za ATCL kwenda India zinaendelea hadi pale mamlaka za hapa nchini zitakapotoa taarifa za kusitisha kwa safari za ndege hiyo nchini humo.

Join our Newsletter