Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 14Article 557308

Habari za Biashara of Tuesday, 14 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

AfDB yaahidi misaada zaidi kwenye ujenzi wa miundombinu na umeme

AfDB yaahidi misaada zaidi kwenye ujenzi wa miundombinu na umeme AfDB yaahidi misaada zaidi kwenye ujenzi wa miundombinu na umeme

BENKI ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeahidi kusaidia zaidi katika miundombinu, uunganishaji wa umeme na kujenga uwezo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB katika nchi za Kenya, Eritrea, Ethiopia, Rwanda, Shelisheli, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda, Cheptoo Amos Kipronoh, ametoa ahadi hiyo alipomtembelea Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Mipango na Miundombinu, Steven Mlote, katika Makao Makuu ya EAC jijini Arusha.

Kipronoh amesema uwekezaji katika miundombinu, uunganishaji wa umeme na kujenga uwezo ndio ufunguo wa maendeleo ya uchumi na kuimarisha mtangamano wa EAC.

Ameipongeza EAC kwa kuwa umoja uliojumuishwa zaidi kati ya jumuiya nane ya kiuchumi za kikanda zinazotambuliwa na Umoja wa Afrika (AU). “AfDB inaipa EAC hadhi ya juu katika malengo yaliyokusudiwa ya jumuiya kubadilisha ukanda huu na kuwa soko moja katika aina mbalimbali za uzalishaji ili kuimarisha ukuaji wa uchumi wa watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema.

Amesema serikali za nchi wanachama wa EAC zimeendelea kujitolea katika mtangamano na kutaka Sekretarieti ya EAC kuendelea kuweka mikakati ya kuondoa changamoto katika kufanya biashara ili kuwezesha upatikanaji wa mnyororo wa thamani katika ukanda huo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa EAC, Mlote, ameishukuru AfDB kupitia mkurugenzi mtendaji wake kwa kuendelea kuunga mkono mtangamano wa EAC na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano wa jumuiya hiyo.

Mlote ameipongeza AfDB kwa kufadhili miradi kadhaa ya miundombinu ikiwemo Barabara ya Arusha-Holili / Taveta-Voi, Barabara Kuu ya Malindi-Mombasa-Lunga Lunga / HorohoroTanga-Bagamoyo inayozunguka Pwani za Kenya na Tanzania, pamoja na barabara ya Athi River-Namanga-Arusha, iliyopunguza muda wa kusafiri kati ya Nairobi hadi Arusha.

Akizungumzia biashara ya ndani ya Afrika Mashariki kutokana na madhara ya kiuchumi yaliyosababishwa na janga la Covid-19, Mlote amesema tangu Mei 2020, biashara imeendelea kuimarika kutokana na hatua mbalimbali za nchi wanachama za kuimarisha usafirishaji EAC.