Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 09Article 556426

Habari za Biashara of Thursday, 9 September 2021

Chanzo: Mwananchi

Air Tanzania yaanzisha malipo ya nauli kwa "Kibubu"

ATCL ATCL

Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imeanzisha mpango wa "kibubu" utakaowawezesha wananchi kulipia kidogo kidogo mpaka atakapo kamilisha malipo ya tiketi yake ya ndege.

Katika mpango huo, mwananchi atatakiwa kuweka Sh50,000 kwa mara ya kwanza na kiasi kinachobakia atatakiwa kulipa kidogo kidogo kwa kiwango anachokimudu mpaka safari yake itakapofika.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Septemba 9 jijini Dar es Salaam, mkuu wa kitengo cha mawasiliano - ATCL, Josephat Kagirwa amesema mpango huo utawawezesha wananchi kupangilia safari zao kwa kulipia tiketi zao kidogo kidogo.

"Tumeweka mpango huu ili kuwasaidia wananchi kuweka fedha kidogo kidogo ili kulipia tiketi ya ndege ndani ya muda ambao amepanga kusafiri," amesema Kagirwa.

Kwa upande wake, meneja wa mtandao wa safari na usimamizi wa mapato katika kampuni hiyo, Edward Nkwabi amesema kwa kuanzia wananchi watafanya malipo ya awali ya tiketi zao (booking) katika ofisi za ATCL lakini baadae wataweza kulipia kwa njia ya benki.

Amesema masharti yanayotumika katika mpango huo ni kama yale yale yanayotumika kwenye tiketi za kawaida. Amesema mteja akiahirisha safari yake, watazingatia vigezo na masharti kabla ya kumpangia safari nyingine.

"Shirika letu lina safari za ndege kila kona ya nchi hii na pia tunakwenda baadhi ya nchi kama vile Burundi. Kwa hiyo, mpango huu utatumika pia katika safari za kimataifa," amesema Nkwabi.

Naye Ofisa Masoko wa ATCL, Grace Magubo amesema kampuni hiyo itatoa zawadi kwa wateja ambao watahamasisha watu zaidi ya watano kutumia mpango huo wa kibubu na zawadi yao ni kujipatia tiketi ya ndege kwa nusu bei ya mahali anakotaka kwenda.