Uko hapa: NyumbaniBiashara2020 10 27Article 513265

Habari za Biashara of Tuesday, 27 October 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Barabara zilivyorahisisha usafirishaji mazao Kagera

Barabara zilivyorahisisha usafirishaji mazao Kagera Barabara zilivyorahisisha usafirishaji mazao Kagera

AMA kwa hakika waliosema barabara ni sawa na mishipa ya damu katika mwili wa mwanadamu kutokana na umuhimu wake wa kuunganisha maeneo mbalimbali na kuboresha uchumi na maisha ya watu hawakukosea.

Pamoja na ukuaji wa uchumi wa Tanzania kuchangiwa na sekta mbalimbali kama madini, utalii, mifugo na uvuvi ubora wa barabara imara nyingi zilizojengwa hususani katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano, umechangia sana kuiharakisha Tanzania kufikia Uchumi wa Kati.

Barabara za mijini na vijijini kwa mfano, zimesaidia sana wakulima katika kusafirisha mazao kutoka mashambani kwenda kwenye masoko mbali na mizigo mengine kama madini, mazao yatokanayo na uvuvi na kadhalika.

Kagera ni moja ya mikoa inayozalisha chakula kwa wingi na barabara ndizo kwa asilimia kubwa hutumika kusafirishia mazao hayo na hivyo kuchangia katika kunyanyua uchumi wa mkoa

Mwaka 2015, moja ya ahadi za mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ni kuboresha miundombinu, ikiwemo ya mijini na vijijini.

Ahadi hizo zimetekelezwa kwa kiwango kikubwa kwani katika halmashauri nyingi za mkoa wa Kagera, barabara nyingi zimejengwa ama kukarabatiwa na nyingine kufunguliwa. Ni mara ya kwanza kwa baadhi ya vijiji kushuhudia lami, jambo ambalo halikutarajiwa.

Barabara ya Omukigando–Omukalinzi iliyopo wilayani Kyerwa ni moja ya barabara ambazo zimesababisha maendeleo makubwa baada ya kukamilika.

Awali kutokupitika kwa barabara hiyo kulisababisha kutenganishwa vijiji na vijiji, jambo ambalo lilifanya wakulima na wanafunzi kushindwa kufika eneo lingine hasa wakati wa kipindi cha mvua.

Mawasiliano kutoka kijiji Omukigando kwenda Omukalizi yalikuwa ni hafifu sana, hakukuwa na uwezo wa kusafisha mazao labda kwa kutumia mitumbwi, huduma za afya, huduma za jamii zilizorota kutokana na kutokuwepo kwa kiunganishi cha barabara.

Shakiru Gabagambi, mkazi wa kijiji cha Omukigando anasema kwa miaka mingi adha ya barabara hiyo muhimu kujaa maji ilikuwa kikwazo cha uchumi na huduma nyingine za jamii lakini mbaya zaidi hata wanafunzi walikuwa hawaendi kabisa shule katika kipindi cha mvua, jambo ambalo lilizorotesha maendeleo.

Kwa miaka ya hivi karibuni barabara hiyo imetengenezwa na wananchi kuondolewa adha hiyo, hivyo hakuna adha tena ya kupita bila hofu yoyote, iwe kipindi cha kiangazi wala masika usafirishaji wa mazao na watu hufanyika bila shida yoyote.

Kashunju Runyogote, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa 2015/2020 na ambaye amekuwa diwani kwa miaka 20 anasema haikuwa kazi rahisi ya kutekeleza mtandao wa barabara kwani wakandarasi walikuwa wanakwamisha barabara, jambo ambalo lilikuwa linawajengea ukuta viongozi wanaotoa ahadi mbalimbali.

“Uchaguzi wa 2015/2020 kwa kweli ni wa historia. Wananchi walituamini na kweli wameshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya miundombinu ya barabara katika wilaya ya Kyerwa ambayo ni wilaya mpya, lakini kwa sasa kuna lami katika makao makuu ya wilaya na miji midogomidogo kama Nkwenda na wengi hawakutegemea kama haya yangefanyika,” anasema Runyogote.

Uboreshaji mkubwa wa miundombinu si katika Wilaya ya Kyerwa pekee bali ukipita maeneo yote ya mkoa wa Kagera utashuhudia mafundi wako kazini usiku na mchana wakijenga makaravati, barabara.

Kwa manispaa ya Bukoba, baadhi ya barabara zilizokuwa kama zimesahaulika zimejengwa au kukarabatiwa. Maeneo ambayo hayakuwa na taa za barabarani sasa zipo. Kwa kifupi mwananchi ambaye alifika Bukoba miaka mitano iliyopita, akifika leo atashuhudia mabadiliko makubwa sana katika sekta ya barabara, ikiwemo uwekaji wa taa za barabarani ambazo zinawaka muda wote.

Uboreshaji na ujenzi wa barabara za vijijini unaendelea kuwanufaisha wananchi wa vijiji mbalimbali ambao kabla ya awamu hii inayomaliza kuingia madarakani walipata adha kubwa ya kutoa mazao yao mashambani kuyafikisha kwenye soko.

Anatoria Kaizirege (53), mkulima wa kijiji cha Izimbya katika kata Izimbya Halmashauri ya Bukoba Vijijini ni mmoja wa wanaothibitisha hili.

Anasema hakukuwa na muunganiko wa barabara kutoka kijiji kimoja kwenda kingine, hivyo magari yalikuwa ya shida tofauti na kipindi hiki ambacho barabara zimetengenezwa na hivyo sasa ukifikisha mazao yako tu barabarani una uwezo wa kuyasafirisha na kuyafisha kokote ambako umesikia soko ni zuri siku hiyo hiyo.

“Uwepo wa uimara wa miundombinu ya barabara haukunufaisha tu wasafirishaji wa mazao, bali pia kumeongeza idadi ya wafanyabiashara kutoka Shinyanga, Geita, Tabora, Mwanza na sehemu mbalimbali wanaokuja kununua mazao yetu kama ndizi, malimau na mazao mbalimbali na hivyo wakulima wengi kunufaika,” anasema.

Kuanzishwa kwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kwa Sheria ya Wakala za Serikali Sura 245 (Executive Agencies CAP 245) na kutangazwa rasmi katika Gazeti la Serikali Na. 211 la tarehe 12/05/2017 ni jambo ambalo limekuwa na manunfaa makubwa kwa nchi.

Wakala umechukua majukumu ya kiutendaji kuhusu ujenzi na matengenezo ya mtandao wa barabaraza vijijini na mijini ambayo yalikuwa yakitekelezwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuratibiwa na Idara ya Miundombinu chini ya TAMISEMI.

Meneja wa Tarura mkoa wa Kagera, Avith Theodory anasema kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 mtandao wa barabara zinazosimamiwa na Tarura umeongezeka kutoka kilomita 5,200 hadi kufikia kilimita 5,885.23, sawa na ongezeko la kilomita 685.23.

Anasema serikali inaendelea na utambuzi wa barabara nyingine zenye urefu wa kilomita 212 na kuzifanyia uhakiki na kwamba baada ya muda mfupi, wanatarajia kuongeza mtandao wa barabara hadi kufikia kilomita 6,097.23 jambo ambalo litazidi kusogeza huduma kwa jamii.

Anasema hakuna halmashauri katika Mkoa wa Kagera ambayo haikunufaika tangu wakala huo ulipoanzisha ambapo kuanzia kipindi cha mwaka 2015 hadi Juni, 2020, jumla ya kilomita 8,008.21, makalavati 465, madaraja tisa mitaro ya urefu wa kilometa 2.53 imejengwa kutokana na fedha za walipa kodi wa Tanzania.

Aidha anasema matengenezo madogo madogo na ukarabati wa miundombinu inayoathiriwa na mvua umekuwa ukifanyika mara kwa mara katika wilaya zote, ikiwa ni pamoja na Biharamulo ambapo kilometa 525.53 zimeshughulikiwa na makalavati 16 huku Bukoba kilometa 811.42 zikiwa zimejengwa au kukarabatiwa, makalavati 28 na madaraja manane.

Wilaya nyingine ni Karagawe, kilometa 2021, makalavati 57; Ngara kilometa 1416.34 makalavati 90; Muleba kilometa 836.76 makalvati 48 na daraja moja; Kyerwa kilometa 1,826.8 makalavati 176 na Missenyi barabara za urefu wa kilometa 475.35 na makalavati 15.

Anasema Dk Magufuli alipotoa ahadi ya kuboresha barabara katika halmashauri za mkoa wa Kagera, ikiwemo baadhi kwa kiwango cha lami wakati anagombea urais mwaka 2015 ilikuwa kama ndoto lakini wananchi wameshuhudia ukweli na kujionea kwamba takribani katika miji midogo yote barabara nyingi za vumbi zimefutika.

Miji imejaa taa zinazomeremeta na wafanyakazi wanavyoingia ofisini ndivyo wanavyotoka kwani hakuna vumbi kama zamani na wanafanya kazi bila bughudha kwani hata wanaofanya kazi hadi usiku wanapita kwenye barabara zenye mwanga na si giza kama zamani.

Khadija Yusuphu (35) anayemiliki duka la dawa za binadamu katika mji mdogo wa Bunazi wilayani Missenyi anasema huko nyuma alikuwa analazimika kuwa anang'arisha duka lake kwa kupaka rangi kila mara kutokana na vumbi lakini kwa sasa ameifuta bajeti hiyo na anafurahia biashara anayoifanya.

“Sijajua nani aliamua kuunda kitu kinachoitwa Tarura kwa sababu ni taasisi ambayo imetufanyia kazi inayoonekana ukizingatia mkoa wetu kipindi cha jua ni jua sana na vumbi kibao. Mimi nilikuwa nahangaika kung’arisha duka kutokana na kuchafuliwa na vumbi kila mwaka huku wakati wa mvua barabara zikiwa hazipitiki lakini sasa hayo yamebaki historia,” anasena.

Meneja wa Tarura mkoa wa Kagera anasema wanatekeleza pia miradi ya barabara katika Wilaya za Kyerwa, Muleba na Missenyi kwa gharama ya Sh bilioni 1.5 zikiwa na urefu wa kilomita tatu.

Anasema hadi sasa miradi miwili katika wilaya za Muleba na Kyerwa imekwishakamilika na mradi mmoja katika Wilaya ya Missenyi umefikia asilimia 70 ya utekelezaji.

Kuhusu fedha Tarura ilizopokea hadi kufanya makubwa ingawa zimekuwa hazifiki asilimia 100 ya bajeti wakati wote, Meneja wa Tarura anasema; mwaka 2016/2017, shilingi bilioni 8.1, mwaka 2017/2018, shilingi bilioni 9.2, mwaka 2018/2019, shilingi bilioni 8.6 mwaka 2019/2020 shilingi bilioni 8.9 na hivyo kufanya jumla ya miradi iliyotekelezwa hadi sasa kugharimu shilingi bilioni 40.8.