Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 08Article 541645

Habari za Biashara ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

DCB yawezesha mikopo ya vikundi

DCB yawezesha mikopo ya vikundi DCB yawezesha mikopo ya vikundi

BENKI ya Biashara ya DCB imesema Watanzania 40,000 wamekuwa wakinufaika kila mwaka na mikopo ya vikundi inayolenga kuwasaidia Watanzania wenye kipato cha chini kupata mikopo yenye masharti nafuu na riba nafuu ili kujikwamua kiuchumi.

Aidha, imebainisha kuwa kwa miaka yake takriban 19 ya uendeshaji, imekuza idadi ya matawi kutoka moja hadi kufikia manane, huku ukuaji huo ukichangia benki kupata faida mfululizo tangu mwaka 2004 hadi 2015.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jana mkoani Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Biashara wa DCB, Zakaria Kapama alisema wamewekeza kwa kiasi kikubwa katika huduma zinazowalenga wajasiriamali walio katika vikundi wakiwa na vikundi vya Vicoba zaidi ya 500.

“Huduma hizi zimeweza kubadilisha maisha na kukuza mitaji ya wengi. Vikundi hivi vinanufaika na huduma bora za kibenki na zenye masharti nafuu kupitia akaunti maalumu za Vicoba, baadhi ikiwemo masharti nafuu ya kufungua akaunti, masharti nafuu katika upatikanaji wa mikopo, masharti nafuu katika uendeshaji wa akaunti hizo,” alieleza.

Aliongeza kuwa DCB imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu na taaluma za kifedha katika vikundi mbalimbali vya wajasiriamali na kushiriki katika kusaidia huduma za kijamii.

Akizungumzia ukuaji wa benki hiyo iliyoanzishwa mwaka 2011, Kapama alisema ukuaji huo umeifanya itoe gawio kwa wanahisa wake katika kipindi chote cha miaka 12. Kutokana na changamoto za mpito, ilipata hasara katika miwili miwili ya 2016 na 2017, lakini imerejea kupata tena faida hadi sasa.

Alifafanua kuwa wamekuwa wakitoa mikopo kwa wajasiriamali hao ambayo imefikia zaidi ya Sh bilioni 100. Alisema walianza kwa mtaji wa Sh bilioni moja lakini kufikia mwaka 2012 walifikisha mtaji wa Sh bilioni 15.

“Hapo mbeleni, Benki ya DCB ambayo imesajiliwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) inatazamia kukuza mizania yake kwa kutumia fursa za ukuzaji biashara na inaazimia kutumia ipasavyo fursa na njia mbadala za utoaji huduma kwa wateja kupitia mitandao, wakala wa kibenki na upanuzi wa mitandao ya matawi na vituo vidogo vya huduma ambapo itasaidia kwa kiasi kikubwa utengenezaji wa mapato kupitia njia ya mapato yasiyo ya riba,” alisema.

Alisema kila mwaka imekuwa ikiingiza bidhaa mpya sokoni na huduma mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya Watanzania zikiwamo zile zinazolenga wafanyabiashara wa kilimo (DCB Sokoni); kugharimia elimu (DCB Skonga); mkopo wa ada; DCB Digital; akaunti za malipo ya serikali, akaunti binafsi, za biashara, za mikopo na za vikundi.

Join our Newsletter