Uko hapa: NyumbaniBiashara2022 01 09Article 584401

Habari za Biashara of Sunday, 9 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Dk Mpango afurahishwa sera ya viwanda SMZ

Dk Mpango afurahishwa sera ya viwanda SMZ Dk Mpango afurahishwa sera ya viwanda SMZ

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema amefurahishwa na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya kuimarisha sera ya viwanda ambayo inakwenda sambamba na dira ya maendeleo ya mwaka 2050 ya kujiimarisha katika kujitegemea na kuongeza ajira kwa vijana.

Mpango alisema hayo wakati alipozindua viwanda viwili vya kushona nguo za wapiganaji pamoja na viatu ambavyo vinamilikiwa na idara maalumu za serikali ya Zanzibar ya Kikosi cha Valantia.

Alisema kuzinduliwa kwa viwanda hivyo ni sehemu ya mikakati ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kuona kasi ya uchumi wa buluu inakwenda sambamba na ujenzi wa viwanda vya aina mbalimbali kwa ajili ya kuvutia wawekezaji na kuzalisha ajira zipatazo 300,000.

Aliutaka uongozi wa viwanda hivyo kuongeza ubunifu unaokwenda na juhudi za kujitangaza na kuingia katika soko kubwa la nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Afrika ya Mashariki na Kati lenye mahitaji makubwa.

Alisema watafanikiwa kuingia katika ushindani wa soko hilo kama watazingatia vigezo muhimu ikiwemo ubora wa bidhaa zinazozalishwa pamoja na gharama nafuu. “Nimefurahishwa na juhudi zenu za uimarishaji wa viwanda hivyo unaotokana na ubunifu wa hali ya juu...Napenda niwahakikishieni kwamba soko la kuuza bidhaa hizi lipo katika nchi za SADC hadi katika Afrika ya Mashariki na nchi jirani za visiwa vya Comoro,” amesema.

Alisema ujenzi wa viwanda vidogo vidogo umenufaisha baadhi ya nchi nyingi ikiwemo za Bara la Asia ikiwemo China ambayo asilimia 90 ya viwanda vyake ni vya kati vyenye kuajiri sehemu kubwa ya wafanyakazi.

Dk Mpango alisema mfano kama huo upo kwa upande wa India ambayo imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa viwanda vidogo vidogo ambavyo kwa asilimia 45, pato la nchi hiyo linategemea uzalishaji wa bidhaa hizo.

''Wakati umefika tujipange zaidi katika ujenzi wa viwanda vya kati ambavyo ni muhimu katika kuzalisha ajira na kuipatia nchi pato kubwa la bidhaa zinazozalishwa kusafirishwa nje ya nchi,'' alisema.

Makamu wa rais amekubali wazo la Idara Maalumu ya vikosi vya SMZ ya kuomba msaada wa wataalamu kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Magereza katika kutoa utaalamu wa kazi za ushonaji na kutengeneza viatu.

''Namuagiza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani kusaidia ujuzi na utaalamu ambao wenzetu wamepiga hatua kubwa katika maeneo ya uwekezaji wa viwanda kusaidia idara maalumu ya SMZ,” alisema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu SMZ, Masoud Ali Mohamed alisema kuwapo kwa viwanda hivyo kutaipunguzia serikali uagizaji wa vifaa vya wapiganaji nje ya nchi na kutumia fedha nyingi.

Aidha, alisema kuwepo kwa viwanda hivyo kumesaidia ajira kwa makundi mbalimbali ikiwemo wapiganaji hadi sekta binafsi za wabunifu wa mitindo ya mavazi yanayokwenda na wakati.

Alisema alipoingia madarakani, serikali ya awamu ya nane ambayo yeye alichaguliwa kuongoza wizara hiyo chini ya idara maalumu, alihakikisha anakamilisha kazi za ujenzi wa viwanda hivyo ambavyo vilianzishwa miaka mingi bila ya mafanikio.

''Awali ilikuwa tunanunua viatu kwa mpiganaji mmoja vinagharimu shilingi 70,000 lakini sasa kwa kuwa tunacho kiwanda chetu wenyewe viatu hivyo vitatugharimu shilingi 35,000,'' alisema. Viwanda hivyo vimegharimu wastani wa Sh bilioni mbili pamoja na kujenga majengo yake