Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 03Article 540700

Habari za Biashara of Thursday, 3 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ewura yatangaza bei kikomo petrol, dizeli 

Ewura yatangaza bei kikomo petrol, dizeli  Ewura yatangaza bei kikomo petrol, dizeli 

MAMLAKA ya Udhibiti na wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei kikomo za mafuta za petroli, dizeli na mafuta ya taa ambapo zimepanda ukilinganisha na mwezi uliopita.

Hayo yamebainishwa juzi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje kupitia taarifa yake kwa umma.

Alisema bei ya rejareja na jumla ya mafuta ya petroli na dizeli yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Alisema kwa mwezi huu, bei ya rejareja ya petroli imeongezeka kwa Sh 80 kwa lita sawa na asilimia 3.7 na dizeli nayo imeongezeka kwa Sh 34 kwa lita sawa na asilimia 1.7.

“Bei ya jumla ya petroli imeongezeka kwa Sh 79.99 kwa lita sawa na asilimia 3.92 na bei ya jumla ya dizeli imeongezeka kwa Sh 34.36 kwa lita sawa na asilimia 1.8.”

“Bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko kwa sababu mwezi uliopita hakuna shehena ya mafuta ya taa iliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Chibulunje.

Chibulunje alisema bei ya jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa mwezi huu kwa mikoa ya Kaskazini ikiwamo ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara zimebadilika ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Alisema kwa mwezi Juni, bei ya rejareja ya petroli imeongezeka kwa Sh 69 kwa lita sawa na asilimia 3.06, lakini kwa dizeli imepungua kwa Sh 116 kwa lita sawa na asilimia 5.27.

“Bei ya jumla ya petroli imeongezeka kwa Sh 68.42 kwa lita sawa na asilimia 3.23 na bei ya jumla ya dizeli imepungua kwa Sh 115.53 kwa lita sawa na asilimia 5.6, bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko,” alisema Chibulunje.

Kwa upande wa mikoa ya Kusini ukiwemo Mtwara, Lindi na Ruvuma, alisema bei za rejareja na jumla kwa mafuta ya petroli na dizeli hazina mabadiliko kwa sababu hakuna shehena iliyopokelewa kupitia Bandari ya Mtwara mwezi uliopita.

Join our Newsletter