Uko hapa: NyumbaniBiashara2022 01 11Article 584875

Habari za Biashara of Tuesday, 11 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Gati jipya Mtwara lapokea meli yake ya kwanza

Gati jipya Mtwara lapokea meli yake ya kwanza Gati jipya Mtwara lapokea meli yake ya kwanza

Baada ya siku tisa na saa tatu kutoka bandari ya Qasim nchini Pakistan, pwani ya Magharibi ya India kama ilivyoripotiwa na MarineTraffic Terrestrial Automatic Identification System, meli ya Star Fighter iliwasili Bandari ya Mtwara nchini Tanzania na kuwa meli ya kwanza ya ukubwa wake kutia nanga katika gati jipya kwenye bahari yenye kina kirefu cha asili.

Star Fighter yenye namba ya usajili baharini (IMO) 9642198 ni meli ya kubeba mizigo mtawanyiko mikubwa iliyojengwa miaka tisa iliyopita (2013) na inasafiria bendera ya visiwa vya Marshall. Ikiwa na urefu wa mita 199.98 na upana wa mita 32.24 ina uwezo wa kubeba tani 61455.

Meli hiyo imefuata makaa ya mawe ya Kampuni ya Ruvuma Coalmine kuyapeleka India.

Gati hilo jipya lililogharimu Sh bilioni 157.8 limemalizika baada ya miezi 22 ya ujenzi.

Akizungumza katika tukio hilo la ujio wa meli Januari 8 mwaka huu bandarini hapo, Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Abdillah Salim anasema kuwa ujio wa meli hiyo na kutia nanga kwenye gati hilo jipya ni matokeo ya serikali katika kuboresha bandari hiyo pamoja na maendeleo ya Kusini mwa nchi.

“Ujio wa meli kama hii kwetu sisi ni faraja kwa sababu biashara inaongezeka na kwa ujumla tunafanya kazi na Watanzania wengine wote wa Kusini wanapata ajira kwa hiyo sisi tumefurahi kuja kwa meli hii,” alisema.

Aliongeza: “Tusingeweza kupata uzito huu wa tani hizi 59,000 kwa hiyo maboresho ya hapa na ujenzi huu wa bandari mpya ndio umesababisha meli hii iweze kufunga hapa… tunawahakikishia wa Kusini na Watanzania kwa ujumla kuwa tuko tayari kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha maendeleo yanakuwepo.”

Mkurugenzi wa Huduma za Meli na Utekelezaji wa shughuli za kibandari kutoka Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Abdallah Mwingamno anasema ni mara ya kwanza kuleta meli kubwa kwenye gati hilo jipya lililojengwa kwa fedha za serikali.

“Itapakia mzigo huu ndani ya siku saba kulingana na vifaa tulivyokuwa navyo kwa sasa kwa hiyo haya ni maendeleo makubwa kabisa ambayo serikali imeyafanya na inaendelea kuyafanya. Kwa maboresho haya tunaamini kwamba hii biashara ya kimeli ya kibandari inaendelea na tunaingiza nchi kwenye ushindani,” anasema.

Bandari ya Mtwara ni mojawapo ya bandari kuu tatu nchini zinazomilikiwa na TPA. Mbali na Mtwara kuna Tanga na Dar es Salaam. Bandari ya Mtwara inasifika kwa kuwa na kina kirefu cha maji na kwamba ilijengwa kati ya mwaka 1948 na 1954.

Ujenzi wa bandari hii uliambatana na ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Nachingwea kulikokuwa na mradi mkubwa wa kilimo cha karanga. Baada ya kushindwa kwa mradi huo, Bandari ya Mtwara nayo ikawa haina matumizi makubwa.

Sasa hivi serikali imeifanyia ukarabati mkubwa na kuanza kuifanya iwe na matumizi hasa kwa kuzingatia uchumi wa mikoa ya Kusini mwa nchi wenye kutegemea zao la korosho na madini mbalimbali yakiwemo makaa ya mawe na chuma.

Ukiangalia matumizi ya sasa na siku za usoni na maboresho ya serikali yaliyofanywa hatua kwa hatua utatambua kwamba bandari ya Mtwara inakuwa lango kuu la uchumi la Kusini mwa Tanzania.

Mradi huo wa miezi 22 hadi kukamilika kwake ulitumia Sh bilioni 157.8 na kuleta hadhi mpya kwa bandari hiyo ambayo ni ya siku nyingi huku ukiongeza uwezo wa bandari hiyo kutoka kusafirisha tani laki 4 mpaka zaidi ya tani milioni 1 za mizigo kwa mwaka.

Aidha, ikiwa na uwezo wa kuhifadhi tani 12,500 za mizigo bandari hii ni moja ya bandari muhimu hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa imeshaanza kuwa na matumizi na maboresho yaliyofanyika hata nchi jirani zinaanza kuangalia uwezekano wa kuitumia ikiwamo taifa la Malawi.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Erick Hamisi anasema kuwa kupitia upanuzi uliofanyika kwenye Bandari ya Mtwara na kuboresha uwezo wake wa awali wa tani laki nne kufikia tani milioni moja kumeifanya iwe na uwezo wa kupokea na kusafirisha mizigo mingi na kuleta fursa ya uchumi wa Kusini na Watanzania wengine kwa ujumla kwani mzunguko wa fedha utakuwa umeongezeka hivyo kutoa tija kwa uchumi wa taifa na watu wa Mtwara.

Upanuzi wa bandari hiyo umefanya uchumi mkubwa wa Kusini, zao la korosho, kutumia bandari hiyo kwa kuleta viuatilifu na pia kutumika kupeleka korosho nje. Mwaka jana meli ya Greentec ilikuwa meli ya kwanza kubwa kupakia korosho kwa msimu wa 2021/22 na ilipakia tani 18,800 za korosho za Kampuni ya Sbatanza kuelekea nchini Vietnam.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya anasema kwamba uboreshaji wa bandari hiyo umeongeza mizigo mbalimbali bandarini hapo na mikakati ya serikali ni kuhakikisha bandari inakuwa na uwezo wa kufanya kazi ya kusafirisha mizigo mingi inayokwenda maeneo mbalimbali nchini na duniani kote.

Aliyekuwa Kaimu Meneja wa Bandari wakati meli hiyo inawasili, Norbert Kalembwe anasema meli hiyo ya kwanza kubeba korosho iliwasili Desemba 15, 2021 na ilitumia siku tano kupakia korosho hizo.

“Bandarini sasa hivi mzigo ambao tumepokea tani elfu ishirini na mbili na zaidi na hii meli inachukua tani elfu kumi na nane na mia nane kwa hiyo upo mzigo ambao utaendelea kuletwa na tutaendelea kupokea meli zingine zaidi ila sasa hivi tunayo Kampuni ya Sbatanza,” anasema Kalembwe.

Katika mazungumzo wakati huo alisema kwamba bandarini hapo palikuwa na takribani tani elfu ishirini na mbili za korosho kutoka Kampuni ya Sbatanza ambazo zimehifadhiwa zikisubiri kusafirishwa.

Mmoja wa vijana ambao hufanya kazi ya kupakia mizigo melini, Yusufu Masudi pamoja na kuipongeza serikali alisema: “Ombi letu kubwa sisi kama vijana bandari hii iwe ‘bize’ muda wote katika kusafirisha bidhaa tofauti kama ilivyo kwa bandari za wenzetu Tanga na Dar es Salaam ili tupate ajira endelevu badala ya kusubiri korosho peke yake na hii itasaidia kupitia bandari hii mkoa huu wa Mtwara kuzidi kuwa na heshima.”

Maboresho katika bandari hiyo kumefanya ipate wageni na miongoni mwao ni Naibu Balozi wa Jamhuri ya Malawi nchini Tanzania, Deborah Mitawa aliyefika bandarini hapo kuona kama nchi yake inaweza kutumia bandari hiyo kusafirishia bidhaa zake. Balozi Mitawa katika mazungumzo anasema atawasiliana na watu wa kwao kuanza matumizi ya bandari hiyo.

Kalembwe anasema baada ya maboresho hayo bandari iko tayari kuhudumia mzigo wa Malawi kwa sababu iko katika eneo zuri na inaweza kuhudumia kwa gharama ndogo nchi ya Malawi, inawezesha meli kuja moja kwa moja na kufunga na kupakua mzigo lakini pia umbali wa kutoka Mtwara kwenda Malawi ni mfupi ikilinganishwa na Bandari ya Dar es Salaam.

Inaelezwa kwamba kuboreka kwa Bandari ya Mtwara na kufunguka kwa Korido la Kusini inatoa uwezo kwa Meli kubwa za magari kutokea nchini Japan na kwa magari yote yanayoelekea Kusini kushushiwa Mtwara.

Maboresho yaliyofanywa pia yaligusia maeneo ya kuhifadhi kemikali na hiyo iliwezesha meli kubwa ya MV YASEMIN ikiwa na tani 2,850 ya viuatilifu vya korosho kwa msimu wa 2021/2022 kutia nanga na kupakua shehena yake. Ujio wa meli hizo unaonesha wazi kwamba, Bandari ya Mtwara sasa ina uwezo mkubwa wa kuhudumia meli za aina hiyo na yote hayo ni matokeo ya uboreshaji wa huduma za bandari hiyo.

Kampuni inayojihusisha na uagizaji, usambazaji wa viuatilifu katika mazao mbalimbali nchini (BENS AGROSTAR COMPAN LIMITED) imeipongeza serikali kwa kuboresha Bandari ya Mtwara kwani inaleta hamasa kubwa kwa wafanyabiashara kuitumia.

Waziri Mawasiliano, Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rahma Kassim Ally ambaye hivi karibuni alitembelea Bandari ya Mtwara ili kujionea maendeleo pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na serikali katika upanuzi wa gati uliogharimu zaidi ya Sh bilioni 157 alitaka bandari hiyo kujitangaza ili iendane na gharama ya uwekezaji huo mkubwa uliofanywa na serikali.

“Nashauri tu kwa upande wenu muitangaze bandari yenu ili ipate harakati zaidi ya kontena na kupata mizigo mingi na mizigo unapokuwa mingi uchumi unazidi kukua kwa hiyo hili la upanuzi wa bandari tunalichukua ili na sisi tuweze kuongeza bandari yetu ya Zanzibar iwe kubwa kama ilivyokuwa hii ya kwenu,” alisema Rahma.

Meneja wa TPA mkoani humo, Juma Kijavara alisema kuwa yadi kwa bandari hiyo mpya ni mita za mraba 75,000 ambazo ni kubwa na kwamba ina uwezo wa kuhifadhi meli kubwa zisizopungua tano jambo ambalo haliwezi kupatikana katika bandari nyingine.