Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 05 05Article 536641

Habari za Biashara of Wednesday, 5 May 2021

Chanzo: ippmedia.com

Infinity, Letshego zazindua huduma mpya ya mikopo ya ujenzi

Infinity, Letshego zazindua huduma mpya ya mikopo ya ujenzi Infinity, Letshego zazindua huduma mpya ya mikopo ya ujenzi

Akizungumza wakati wa kutia saini ya ushirikiano huo kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Infinity Real Estate Tumaini Mtei na Mkurugenzi wa Biashara wa Letshego Dr. Goodluck Meena Jijini Dodoma, Meneja Biashara wa Infinity, Lulu Nzalalila alisema ushirikiano huo utachangia wateja wengi kupata huduma za kitaalamu zaidi za ujenzi kwa bei nafuu.

“Watu wengi wanafikiri huduma za kitaalamu zinazotolewa na kampuni kama yetu ni ghali lakini sio kweli kwani huduma hii tunayozindua leo inawalenga wateja wenye vipato mbalimbali ambao watashauriwa ipasavyo kuhusu mkopo huu,” alisema

Alisema baadhi ya huduma ambazo mikopo itatolewa ni pamoja na ujenzi wa nyumba kuanzia mwanzo, uendelezaji wa viwanja, umaliziaji wa ujenzi na ukarabati.

“Watu wengi wana viwanja lakini hawana fedha za kuviendeleza au kufanya ujenzi. Tuna vifurushi mbalimbali kwa wateja wenye vipato mbalimbali ambapo pia marejesho yatakuwa na unafuu ili watu wengi zaidi waweze kutumia huduma hii ili waweze kujenga na kumiliki nyumba,” alisema.

Alisema huduma hii itahakikisha wateja wanapata suluhu mbalimbali kwa bei nafuu kwenye suala la vifaa vya ujenzi."Natoa wito kwa Watanzania wajenge utamaduni wa kuomba mikopo ya nyumba kwani hii itasaidia kuongeza idadi ya wanaomiliki nyumba kama ilivyo katika nchi zingine," alisema na kuongeza;

“Kwa kupitia huduma hii tunataka kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanamiliki nyumba na pia wanaweza kukopesheka katika mabenki na taasisi nyingine za kifedha, 

Kwa upande wake, Meneja Biashara wa Benki ya Letshego, Ruth Mpangala, alisema benki hiyo inafarajika kuwa sehemu ya ushirikiano na Infinity Real Estate Dodoma na kuwataka wateja watumie huduma hiyo  ili wajipatie mikopo ya ujenzi.

“Hii ni hatua nzuri mno na sisi Letshego tutahakikisha wateja wanapata huduma bora ikiwemo marejesho yenye unafuu kwa wateja wenye vipato mbalimbali ili kuhakikisha wakazi wengi zaidi wa Dodoma wanafaidika na huduma hiyo,” alisema.

Alisema moja ya vigezo watakavyozingatia ni mteja mwenye kipato cha uhakika hata kama ni kidogo kwani kuna vifurushi mbalimbali kwa wateja mbalimbali na kuongeza kuwa wateja watatambulishwa kwa Benki ya Letshego na kampuni ya Infinity.

Join our Newsletter