Uko hapa: NyumbaniBiashara2020 10 13Article 511948

Habari za Biashara of Tuesday, 13 October 2020

Chanzo: habarileo.co.tz

Jiko sanifu linalotumia umeme kidogo kuokoa fedha, misitu

Jiko sanifu linalotumia umeme  kidogo kuokoa fedha, misitu Jiko sanifu linalotumia umeme kidogo kuokoa fedha, misitu

UTAFITI uliofanywa na taaisi ya kuendeleza Huduma za Nishati Endelevu (TaTEDO) kwa kushirikiana na kampuni ya Gamos pamoja na vyuo vikuu vya Surrey na Loughbrough vya nchini Uingereza umeonesha kuwa maendeleo ya teknolojia yamewezesha upatikanaji wa vifaa vya kupikia vyenye ufanisi mkubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita Mkurugenzi Mtendaji wa TaTEDO, Estomiah Sawe anataja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na Jiko Sanifu la Umeme lenye presha (JULEP) ambalo linatoa fursa kubwa ya kuunganisha juhudi za kusambaza umeme, kuwasha taa na kwa kupikia kwa gharama ndogo.

“Kutegemeana na chanzo cha umeme, matumizi ya umeme kupikia kwa kutumia Julep sasa yanatambuliwa kuwa ndio suluhisho sahihi na endelevu la nishati ya kupikia hapa nchini Tanzania,” anasema.

Sawe anasema kwa kutumia jiko hilo sanifu na vifaa vingine, kaya zetu zenye umeme zinaweza kuutumia umeme kwenye kupika kwa gharama nafuu kuliko mkaa na gesi.

Anasema, Julep ni jiko la umeme linalopika kwa kutumia joto na presha ya mvuke unaokusanywa ndani ya sufuria. Jiko hili hutumia nishati kidogo sana kuivisha chakula kwa muda mfupi na kuhifadhi ladha, hivyo huokoa fedha, muda, afya na mazingira.

Anasema linaweza kupika kwa njia ya kuchemsha, kuoka, mvuke (steam cooking) na kukaanga. Julep linajumuisha vifaa vya kupikia tunavyovifahamu ambavyo ni kasha la kuhifadhi joto, jiko la umeme pamoja na sufuria.

Anasema ili usambazaji wa Julep uenee sehemu kubwa ya nchi, kunahitajika kuwepo na sera wezeshi, uwekezaji kwenye teknolojia hii na ushirikiano kwenye sekta mbalimbali zinazohusika na nishati.

“Kwa sasa hivi, kutumia umeme kupikia hata kama unao nyumbani kwako inaonekana kama kitu kisichowezekana kutokana na gharama. Lakini kwa Julep sasa inawezekana,” anasema.

Anafafanua kuwa ili watu wengi waweze kupata teknolojia mambo kadhaa yanapaswa kufanyika ambayo ni pamoja na kuhamasisha wajasiriamali ili waweze kuagiza majiko sanifu ya umeme yenye presha kwa wingi. Lakini analosisitiza Sawe ni serikali kupunguza au kuondoa kabisa kodi ili wananchi wengi zaidi waweze kunua majiko haya.

Sawe anashauri kwamba endapo soko likikua, ni vyema kujenga kiwanda hapa nchini cha kuyazalisha majiko hayo kwa kutumia makampuni ya wananchi wenyewe na kuendeleza soko na mitandao kwa ajili ya kuyasambaza na kutoa huduma kwa wateja kama pembejeo, ufundi na kuwawezesha wajasiriamali.

Kwa upande wake, meneja wa kampuni ya Sustainable Energy Enterprise Ltd, Shima Sago, anasema kuwa soko rasmi la nishati ya kupikia hapa Tanzania halijaendelezwa na kwa sasa linajumuisha zaidi kuni na mkaa.

Anasema serikali imejiwekea lengo la muda mrefu la kuhakikisha zaidi ya asilimia 75 ya kaya zote nchini zinatumia nishati na teknolojia za kisasa kupikia ifikapo mwaka 2030.

Anasema nishati na teknolojia zinazopewa msukumo zinajumuisha gesi (LPG), bayogesi, umeme na majiko sanifu. Hata hivyo, anasema bado juhudi zinazofanyika hazijaleta matokeo ya kuridhisha.

Akitolea mfano, Sago anasema kuwa bayogesi haijaweza kutumiwa na wananchi wengi kutokana na gharama za awali za kutengeneza mtambo kuwa kubwa na changamoto ya kuhudumia kila siku.

Pia anasema kuhusu majiko ya kawaida ya umeme yalizoeleka, licha gharama za kuyanunua kuwa kubwa, yanasababisha gharama za bili kuwa kubwa na hivyo wannachi kushindwa kuyapiki.

Anasema kuna juhudi zimefanyika kukuza matumizi ya majiko sanifu ya kuni na mkaa, lakini kutokana na bajeti na uwekezaji mdogo kwa wajasiriamali na watumiaji, juhudi hizi hazijafanikiwa sana.

Anasema kutegemea kuni na mkaa ni hatari kwa misitu yetu hasa kwa kuzingatia kwamba kunakuwa pia na ongezeko la watu kila mwaka.

“Ni habari njema kusikia ujio wa jiko sanifu la umeme lenye presha la Julep linalotumia umeme kidogo na habari hii inazidi kuwa njema zaidi kutokana na mpango wa serikali wa kuzidi kusambaza umeme vijijini,” anasema.

Katika kampeni zake, Rais Magufuli amekuwa akisema kwamba miongoni mwa vijiji 12,268, vijiji zaidi 9,000 vimeshapatiwa umeme na kwamba vijiji 2,000 na ushei vilivyobaki vitapatiwa pia umeme akirejea madarakani.

Akizungumzia faida za Julep kulinganisha majiko mengine, Sawe anasema kwa kutumia jiko hilo sanifu la umeme mtu ataweza kupika kwa chini ya uniti mbili za umeme kwa siku, sawa na Sh 720 kwa watumiaji wa umeme wa Gridi ya Taifa.

Anasema mbinu za kupika zinaweza kuwa ni kichocheo kikubwa katika matumizi sanifu ya nishati na hivyo kupunguza matumizi ya umeme hadi uniti moja kwa siku.

Anasema kwa familia ya kawaida watu watano hadi wanane, wastani wa gharama ya kupika vyakula vyote kwa jiko sanifu la umeme lenye presha ni Sh 21,900 kwa mwezi.

Anadai kwamba chakula kilichopikwa kwenye jiko sanifu la umeme lenye presha hubaki na ladha bora zaidi kulinganisha na kilichopikwa kwenye gesi au mkaa.

Pia anasema jiko hilo sanifu linatunza virutubisho vya chakula vizuri zaidi kulinganisha na aina nyingine za majiko.

Ninajua kipimo ambacho wengi wanatumia kuhusu gharama za jiko ni kwenye maharage ambayo kwa kawaida huchukua muda mrefu kidogo kuiva kulinganisha na aina nyingine za vyakula kama samaki na nyama. Lakini kwa kutumia Julep gharama za kupika kilo moja ya maharage ni wastani wa uniti 0.4 hadi 0.5 (sawa na shilingi 140 mpaka 175), anasema.

Anasema mbali na kuokoa fedha kwa takribani asilimia 85 kulinganisha na majiko mengine, jiko hilo huokoa pia muda wa kupika.