Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 11 16Article 571702

Habari za Biashara of Tuesday, 16 November 2021

Chanzo: IPPmedia

Jinsi TCC ilivyotoa ajira kwa maelfu nchini

Jinsi TCC ilivyotoa ajira kwa maelfu nchini Jinsi TCC ilivyotoa ajira kwa maelfu nchini

Kampuni ya sigara nchini TCC, imesema moja ya mafanikio yake ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake ni pamoja na kutoa ajira kwa maelfu ya watanzania.

Kampuni hiyo ilizinduliwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere Desemba 4, 1961, siku chache tu kabla ya Tanzania kutangazwa kuwa taifa huru na Uingereza.

Hayo yalibainishwa jana mkoani Dar es Salaam na Patricia Mhondo, Mkurugenzi Uhusiano na Mawasiliano wa TCC wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo vya habari katika kiwanda cha kuzalisha sigara.

Patricia alisema kwa sasa TCC imetoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania 2,749 kati ya ajira takribani 40,000 zinazotolewa na kampuni mama ya JTI duniani.

Mbali na utoaji wa ajira za maelfu kwa Watanzania, alisema TCC imeendelea kujipanua na kutoa mchango mkubwa kwa serikali, ikiwamo kodi.

Alisema: “Tunapoendelea kujitanua, mchango wetu kwa serikali pia umeongezeka na kufikia wastani wa kodi ya zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Patricia, mchango na utendaji wa TCC kwa ujumla umekua mara kwa mara kwa miaka mingi na kufikia uwezo wa uzalishaji wa vijiti vya sigara bilioni 10 kwa mwaka, huku ikidumisha wastani wa hisa asilimia 90 ya soko katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Kwa upande wake, Michael Bachan, Mkurugenzi Mkuu wa TCC (Plc) alisema: “Mwaka huu, TCC (Plc) inaadhimisha miaka 60 ya kazi kwa mtindo huku tukiendelea kurekodi matokeo bora. Licha ya changamoto za Uviko-19 katika kipindi cha miaka 2 iliyopita, TCC (Plc) imerekodi utendaji bora katika nusu ya kwanza ya mwaka.

Alisema kiasi cha mauzo ya ndani na nje kimeongezeka kwa asilimia 16.5 na asilimia 3.7 kwa mtiririko huo huku kiasi cha jumla kikiongezeka kwa asilimia 12.5.

Bachan, alisema ukuaji huu wa kiasi unaonyesha nguvu ya muundo wa usambazaji wa ndani uliorekebishwa. “Kwa matokeo haya, kampuni ina matumaini kuhusu matokeo ya nusu ya pili ya mwaka."

Alisema wanaamini kuwa hilo limewezekana kwa sababu ya kujitolea bila kuyumba kwa wafanyakazi wao, ambao ni mali kwa shirika na mchango muhimu kwa biashara.

Bachan aliongeza: "TCC (Plc) inazingatia kuwekeza katika afya ya watu, ustawi na vipaji na kwamba imeboresha mienendo ya kufanya kazi na kuinua viwango ambavyo vimekubalika kitaifa na kimataifa.

Alisema mwaka 2021, kampuni ilitambuliwa kama ‘Mwajiri Bora’ kwa mwaka wa nne mfululizo na Taasisi ya Mwajiri Bora.

Aidha, alisema ilipata cheti cha kiwango cha dhahabu katika cheti cha 'Wawekezaji katika Watu', tathmini ya jinsi kampuni inavyotoa utamaduni ulioboreshwa wa kufanya kazi kwa kuwaweka watu wao mbele na kuweka uwiano sahihi wa maisha ya kazi kwa ajili ya kujenga afya bora na yenye nguvu zaidi, jamii yenye furaha zaidi.

Aliongeza kuwa kwa miaka mingi, uongozi imara na uwekezaji thabiti kwa watu umefungua njia kwa Watanzania 25 kufanya kazi za kimataifa katika nyadhifa mbalimbali nje ya Tanzania (mfano kama Makamu wa Rais, Wakurugenzi na Mameneja) katika nchi mbalimbali zikiwamo Uswisi, Uingereza, Canada, Nigeria, Zambia, Malawi, Sudan, Geneva, Iran, Jordan, Ethiopia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Kadhalika, alisema TCC inaendelea kutoa kwa jamii moja kwa moja na kwa njia nyingine kupitia ushirikiano na washirika wa kijamii na kitamaduni kukuza mageuzi kamili na endelevu ya maisha.