Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 03Article 540709

Habari za Biashara ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Jinsi ya kutumia madume ufugaji wa kisasa

Jinsi ya kutumia madume ufugaji wa kisasa Jinsi ya kutumia madume ufugaji wa kisasa

“Kwa ufugaji wenye tija, ng’ombe mmoja dume anapaswa atumike kutoa mbegu kwa maana ya kupanda majike 25 tu, kwa msimu wa joto. Dume huyo anatakiwa ahamishwe kila baada ya miaka miwili ili asiharibu kizazi kwa kuwazalisha watoto wake.

“Ndivyo wataalamu wanavyoelekeza ikiwa ni jitihada za kutusaidia kutoka kwenye ufugaji wa asili kwenda wa kisasa ambao una faida lukuki ikilinganishwa na wa kienyeji,” anasema mmoja wa wafugaji wadogo katika wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Maige Shija.

Shija anasema wafugaji hao wamekua wakifundishwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kituo cha Mabuki-Mwanza namna ya kutumia teknolojia mbalimbali, ikiwemo ya ‘madume yaliyoboreshwa’ ili kupata kizazi chenye nguvu na mazao mengi, kwa faida mbalimbali ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Anasema taasisi hiyo tayari imefanya utafiti wa aina mbalimbali za madume ya ng’ombe, ikiwemo ‘Ankole’ na ‘Mpwapwa’ na kukuta yanafaa kueneza kizazi cha ng’ombe chotara kwa wafugaji wa Kanda ya Ziwa ili kuchochea ufugaji wenye tija.

Ankole na Mpwapwa wamekua na sifa zinazoendana, ikiwemo ya ustahimilivu wa hali ya hewa na ndama wake huzaliwa wakiwa na uzito mkubwa.

Wastani wa uzito wa kuzaliwa kwa ng’ombe aina ya ankole ni kilo 25 kwa ndama dume na kilo 22 kwa ndama jike, ikilinganishwa na kilo18.8 na 17.5 kwa ndama dume na jike wa ng’ombe wa asili.

Chaguo lake binafsi ni ankole ambao kwa Tanzania hufugwa katika mikoa ya Geita na Kagera.

Anaendelea kueleza faida za dume bora kwamba husaidia mifugo yake kuzaliana kwa kasi kwani ndama chotara hukua na kupevuka haraka ambapo huanza kuzaa akiwa na umri wa miaka miwili na nusu ikilinganishwa na miaka mitatu kwa ndama wa ng’ombe wa asili.

Kuna ongezeko la maziwa kutoka lita mbili kwa siku alizokua akipata kutoka ng’ombe asili, hadi lita sita mpaka nane kwa ng’ombe chotara aliyezaliwa kutokana na mchanganyiko wa dume la Mpwapwa jike asili.

“Ni kwa mtindo huo hata ndama dume hufikia uzito wa kuingia sokoni kuuzwa kama mbegu au kwa kuchinjwa akiwa na umri takribani huohuo wa miaka miwili. Hata hivyo, nakiri kwamba tofauti hiyo kati ya ng’ombe wa asili na chotara huchangiwa zaidi na malisho bora,” anasema na kuthibitisha kwamba:

Chotara mwenye umri wa mwaka mmoja huuzwa kwa kiasi cha Sh 800,000 ikilinganishwa na Sh 300, 000 ya ng’ombe wa asili, lakini umri uleule.

Mfugaji mwingine, Roberth John anasema ng'ombe chotara anafikisha takribani kilo120 kwa muda wa mwaka mmoja ikilinganishwa na kilo 70 za yule wa asili mweye umri sawa.

Anasema hata mwonekano wa chotara huwavutia wateja mnadani na hivyo kuongeza kasi ya mauzo na manunuzi.

“Nazalisha si tu wa kuuza kwa ajili ya kuchinja bali nauza mbegu pia za madume yaliyoboreshwa ambayo yana wateja wengi kuliko wanaoenda kuchinja,” alisema.

Ng’ombe aina ya ankole ana asili ya pembe ndefu lakini ndama wanaozaliwa baada ya mchanganyiko wa mbegu za ankole dume na jike asili huwa na pembe za kimo cha kati.

Faida yake ni kwamba ng’ombe chotara wanakaa wengi zaidi kwenye zizi ilikinganishwa na wale wa pembe ndefu, na hivyo kuwa na wanyama wengi (chotara) kwenye eneo dogo, anasema.

Mbali na madume yaliyoboreshwa, wafugaji wa Misungwi pia ni miongoni mwa wanufaika wa teknolojia ya unenepeshaji mifugo inayosambazwa na Kituo cha Mabuki pia.

Wanasema ni biashara yenye faida kubwa naya haraka kwani hununua ngo’mbe wa asili na kuwalisha chakula chenye virutubisho vyote muhimu kama inavyoelekezwa na wataalamu, na kupata mrejesho ndani ya muda mfupi.

Vyakula hivyo ni vile vyenye virutubisho vya wanga, protini na madini. Ng’ombe pia ni lazima apatiwe maji ya kutosha.

Bei ya kununua ni kati ya Sh 300,000 na Sh 400,000 kwa ng’ombe mmoja na mauzo si chini ya Sh 800,000 baada ya unenepeshaji.

Wafugaji wanaiomba serikali na wadau wengine kuanzisha viwanda vya uchakataji wa mazao ya mifugo katika wilaya yao kutokana na uwepo wa malighafi za kulisha viwanda hivyo baada ya wao kutumia teknolojia mbalimbali za ufugaji bora na wa kisasa.

Walisistiza kwamba maboresho ya ufugaji yanapelekea si tu wingi bali ubora wa mazao ya mifugo, hasa maziwa, nyama na ngozi ambazo ni malighafi muhimu kwa viwanda.

Mtafiti wa Taliri katika kitengo cha wanyama wadogo wanaocheua, Alphonce Kamgisha, anasema si tu ng’ombe bali Kituo cha Mabuki kimefanikisha uwepo wa madume ya mbuzi yaliyoboreshwa.

Utafiti ulifanyika kwa mbuzi aina ya ‘Malya’ au ‘blended’ na kuonyesha kuwa wana uwezo wa kuzaa mapacha.

Aina hiyo ya mbuzi ilitokana na mchanganyiko wa vizazi vitatu tofauti, ikiwemo cha ‘kienyeji’ (asilimia 15) kwa sababu wana uwezo wa kustahamili magonjwa, ‘Kamorai’ (asilimia 55) kwa ajili ya maziwa na ‘Boar’ (asilimia 30) kwa ajili ya nyama.

Kamgisha anasema kama ilivyo kwa ng’ombe chotara, mbuzi ‘blended’ pia hukua haraka kwani baada ya mwaka mmoja na nusu dume huweza kufikisha wastani wa kilo 32.5 ikilinganishwa na kilo 17.5 za dume la kienyeji.

Bei ya mbuzi chotara mwenye umri kati ya miezi nane hadi mwaka mmoja ni Sh 70,000 hadi 80,000 na wa kienyeji ni 35,000 hadi 40,000 wa umri huohuo.

“Na mbuzi Malya huchungwa kienyeji lakini tunasisitiza wajengewe banda bora linalofanyiwa usafi kila siku na lisiloruhusu baridi kupita wala unyevu ili kuzuia magonjwa na visumbufu vya mifugo kama vile viroboto na chawa,” anasema.

Kama ilivyo kwa ng’ombe, na kwa mbuzi pia inatumika kanuni ni ile ile ya dume moja kwa majike 25, kwa msimu wa joto, ili kuwa na mazao ya kutosha na kizazi chenye nguvu.

Na kutokana na kasi ya kuzaliana kwa mbuzi ambayo ni mara tatu kwa miaka miwili, inashauriwa dume likae na majike kwa mwaka mmoja tu ili lisiharibu ukoo wake kwa kuwazalisha watoto wake.

Mfugaji Joseph Charles, mwenye zaidi ya mbuzi 100 anasema mojawapo ya faida ya mbuzi chotara ni mfugaji kuamua kuwafanya kuwa ama wa maziwa tu au nyama.

Binafsi amewafanya kuwa wa nyama kwani alihitaji kipato cha kumwezesha hasa kutoka katika makazi duni na kwenda ya kisasa.

HabariLeo lilishuhudia nyumba yake ya pili ikiwa hatua za mwisho za ujenzi, ambapo anasema zote mbili amezijenga kutokana na mauzo ya mbuzi.

Anauza mbuzi chotara kwa Sh 150, 000 kutoka Sh 50, 000 aliyokua akipata kwa mbuzi wa asili.

Kaimu Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Ziwa, Dk Heriel Massawe anasema pamoja na jitihada za kubadili ufugaji wa asili kwenda ulioboreshwa, bado mifugo ya asili ina umuhimu wake, ikiwemo ustahimilivu wake kwa magonjwa na ukame.

Anasema pamoja na tafiti zinazoendelea za kuufanya ufugaji kuwa wa tija zaidi, vizazi asili vya mifugo vitaendelea kuwepo kwa sababu mbalimbali za kitaalam lakini pia kwa fahari ya watanzania.

Join our Newsletter