Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 14Article 542551

Habari za Biashara of Monday, 14 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kahawa ya Tanzania kuonjwa China leo

Kahawa ya Tanzania kuonjwa China leo Kahawa ya Tanzania kuonjwa China leo

UBALOZI wa Tanzania nchini China, leo unatarajiwa kuandaa hafla ya kuonja kahawa ya Tanzania itakayofanyika kwa siku tano.

Hivi karibuni Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ilisema kahawa ya Tanzania itatangazwa kwenye soko la China kuanzia leo hadi Juni 18.

Taarifa ya Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TanTrade, Daniel Biah, ilieleza kuwa Ubalozi wa Tanzania China unaratibu hafla ya kuonja kahawa ya Tanzania nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa umma, ubalozi utashirikiana na Idara ya Biashara ya Jimbo la Hunan na kampuni zinazonunua kahawa nchini China.

Biah alisema kampuni zinazonunua kahawa kutoka sehemu mbalimbali duniani zinatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo jijini Changsha.

Tantrade ilisema hafla hiyo ni sehemu ya matukio ya awali kabla ya maonesho ya biashara na uchumi ya China na Afrika yanayotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu.

“Wazalishaji na wauzaji wa kahawa nchini wanahimizwa kushiriki halfa hiyo ili kutangaza kahawa ya Tanzania kwa kutuma sampuli za kahawa kwa ajili ya zoezi la uonjaji,” alieleza taarifa hiyo.

Biah alizitaja sampuli zinazohitajika kuwa ni washing bean, nitro dry bean, anaerobic process bean, honey white yellow black bean, red wine treatment bean.

Wiki iliyopita Balozi wa Tanzania China, Mbelwa Kairuki alitangaza kuwa kahawa ya Tanzania imeanza kuuzwa nchini humo kwenye soko lenye watumiaji milioni 760.

“Ni jambo la faraja kuona jitihada za kuitangaza kahawa ya Tanzania katika soko la China-zimeanza kuzaa matunda. Kahawa yetu imeanza kuuzwa China kupitia "Taobao E-Commerce Platform" yenye watumiaji milioni 760. Ninaipongeza kampuni ya Tanzanite Coffee Ltd kwa kuchangamkia fursa,” aliandika Kairuki kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter.