Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 08 14Article 551497

Habari za Biashara of Saturday, 14 August 2021

Chanzo: Tanzaniaweb

Kampuni 50 kutoka Misri kuwekeza Tanzania.

Kampuni ya Elsewedy Electric kutoka Misri Kampuni ya Elsewedy Electric kutoka Misri

Rais na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Elsewedy Electric kutoka nchini Misri, Mhandisi Ahmed El Sewedy El Sewedy ambaye kampuni yake ni miongoni mwa zinazojenga mradi wa kuzalisha umeme katika Bwawa la Mwalimu Nyerere, amesema anatarajia kuwekeza katika ujenzi wa reli ya kisasa na katika kipindi cha miaka miwili, atahamasisha kampuni takribani 50 kutoka Misri ili kuwekeza nchini Tanzania.

Kampuni ya Elsewedy Electric kutoka Misri, imesema imevutiwa na Uongozi wa Rais Samia Suluhu na kuamua kuunga mkono kwa kuwekeza zaidi nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu, Ahmed El Sewedy alisema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia katika Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma, jana.

“Amesema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yanayoendelea kuwekwa na serikali, wameamua kuunga mkono na kuwekeza zaidi kwa kujenga eneo la viwanda lenye ukubwa wa mita za mraba milioni mbili ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha mbolea,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa upande wake, Rais Samia amemshukuru El Sewedy na kumhakikishia kuwa serikali itampa ushirikiano katika kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo kwa muda muafaka.

Alimjulisha kuwa kwa sasa Tanzania inapitia sheria na sera zake mbalimbali ili kujenga mazingira mazuri zaidi ya biashara na uwekezaji.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sewedy alisema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yanayoendelea kuwekwa na Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia, ameamua kuwekeza zaidi nchini Tanzania.