Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 06 04Article 540946

Habari za Biashara of Friday, 4 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Kongano la viwanda vya korosho kujengwa Masasi  

Kongano la viwanda vya  korosho kujengwa Masasi   Kongano la viwanda vya korosho kujengwa Masasi  

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema serikali imetenga Sh bilioni moja katika mwaka wa fedha 2021/22 ili kuanza ujenzi wa kongano katika eneo la Masasi mkoani Mtwara kwa ajili ya kubangua korosho.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Agnes Hokororo (CCM), Kigahe alisema ni kweli kwamba mazao ya kilimo yanatakiwa kupata masoko na kuongezewa thamani ya kuchakatwa katika viwanda vya ndani ya nchi.

“Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana serikali inataka kujenga kongano ili kuhakikisha wajasiriamali wadogo wanashiriki katika kubangua korosho katika eneo hilo,” alisema.

Kigahe alisema utaratibu huo umewekwa baada ya kuona viwanda vidogo vinakosa malighali kwa ajili ya kubangua korosho na ndiyo maana vinapewa nafasi ya kununua korosho katika minada mikubwa.

Alisema kampuni hizo zinaruhusiwa kushiriki kununua korosho katika minada mikubwa kwa ajili ya viwanda vyao vya kubangua korosho, lakini zikitosheka na malighafi hiyo ndipo zinaruhusiwa kuuza malighafi hizo nje ya nchi.

Katika swali lake, Agnes Hokororo alitaka kujua ni lini serikali itaanza ujenzi wa kongano hilo hasa baada ya kuwa tayari imeshatenga Sh bilioni moja kwa ajili ya kulijenga katika eneo la Masasi.

Mbunge huyo pia aliuliza serikali ina mpango gani kudhibiti uuzaji wa korosho ghafi nje ya nchi, badala ya viwanda hivyo kununua korosho katika minada na kuuza nje bila kubangua na kuongeza thamani ndipo iuzwe nje ya nchi.

Kuhusu swali lingine la Mbunge Hokororo la ni lini serikali itafufua viwanda vya korosho vilivyopo katika wilaya za Masasi na Newala ili kuchakata korosho ghafi na kuongeza bei ya zao hilo, Kigahe alisema, wilaya za Masasi na Newala zilikuwa na viwanda vitatu vya kubangua korosho vilivyokuwa vikimilikiwa na serikali na kubinafsishwa.

Viwanda hivyo, ni Masasi Cashew, Newala I Cashew na Newala ll Cashew.

Alisema kiwanda cha korosho cha Masasi kilichopo Masasi kilibinafsishwa na kuuzwa kwa Kampuni ya BUCCO Investments Holdings Limited ambayo ilishindwa kukiendesha kutokana na Benki ya CRDB kuzuia mali za kiwanda baada ya kiwanda kushindwa kurejesha mkopo waliokopa.

Alisema baadaye kiwanda kiliuzwa na Benki ya CRDB kwa Kampuni ya Micronix Export Trading Co. Ltd kwa njia ya mnada.

Alisema Kampuni ya BUCCO Investments Holdings Limited haikuridhika na utaratibu uliotumika kuuza kiwanda hicho, ikafungua kesi mahakamani na kuishtaki Benki ya CRDB.

“Kesi hiyo bado ipo mahakamani hivyo uendelezaji wa kiwanda hicho umesimama kusubiri uamuzi ya mahakama,” alisema.

Naibu Waziri alisema kiwanda cha Newala I Cashew kilinunuliwa na Kampuni ya Micronics System Ltd na kwamba kinaendelea kufanya kazi.

Alisema Kiwanda cha Newala II Cashew Factory kilinunuliwa na Kampuni ya Agrofocus (T) Ltd.

“Tangu kibinafsishwe, kiwanda hicho hakijawahi kufanya kazi, hivyo mwaka 2019 kilirudishwa katika umiliki wa serikali chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina,” alisema.

Kiwanda hicho kama vilivyo viwanda vingine vilivyorudishwa serikalini kipo katika utaratibu wa kupatiwa mwekezaji mwingine mwenye uwezo wa kukiendeleza.

Alisema katika mpango wa serikali wa kujenga Kongano inatarajiwa kwama hatua hiyo itasaidia ubanguaji wa korosho kwa maeneo yote ya Masasi na Newala.

Aidha, alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na sekta binafsi inaendelea kuweka mazingira ya ufufuaji na ujenzi wa viwanda nchi nzima ikiwemo maeneo ya Masasi na Newala.

Join our Newsletter