Uko hapa: NyumbaniBiashara2021 09 07Article 555853

Habari za Biashara of Tuesday, 7 September 2021

Chanzo: ippmedia

Lake Oil imepigwa faini ya Tsh. Bilioni 3.3 kwa ujenzi bila vibali

Kituo cha mafuta. Lake oil Kituo cha mafuta. Lake oil

​​​​​​​Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeitoza faini ya Sh. bilioni 3.3, Kampuni ya Mafuta ya Lake Oil inayotuhumiwa kujenga vituo vingi vya mafuta maeneo mbalimbali, bila kuwa na vyeti vya Tathmini ya Athari za Mazingira (EIA).

NEMC imemtaka mmiliki wa kampuni hiyo kulipa faini hiyo ndani ya siku 14, kuanzia leo na asipofanya hivyo itatumia sheria kuvifungia vituo vyake vyote 66, nchini.

Hayo yamesemwa Septemba 6, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema wamefikia hatua hiyo baada ya malalamiko ya wananchi wengi katika maeneo, ambayo vituo hivyo vinajengwa.

“Tunaendelea kufanya uchunguzi nchi nzima na wote tutakaowabaini kujenga vituo bila EIA watatozwa faini kama hii, kwa mujibu wa sheria kwasababu tumegundua, kwamba vituo hivi vinaota kama uyoga na hatuwezi kuendelea kubembelezana wakati elimu tumeshatoa sana,” alisema Dk. Gwamaka.

Amesema NEMC imebaini ongezeko kubwa la ujenzi wa vituo vya mafuta, ambavyo katika uchunguzi wao wamebaini kuwa vingi havina vibali vya ujenzi wala vyeti vya EIA.

Dk. Gwamaka alitoa siku saba kuanzia leo kwa vituo vyote, ambavyo vimejengwa bila kuwa na vibali vya EIA kufika kwenye ofisi za NEMC, kwa ajili ya kutoa maelezo kwanini visichukuliwe hatua.

Amesema imepita miaka 17 tangu sheria ipite na NEMC imetoa elimu kupitia njia mbalimbali, lakini wenye vituo vingi wameonyesha ukaidi hivyo muda wa kuchukua hatua kali umefika.

Amesema hakuna asiyeona vituo vya mafuta vinaibuka katika kasi, ambayo ni ya ajabu sasa kwa muda NEMC imekuwa ikijiuliza mbona haioni vituo hivyo kwenda kujisajili kupata EIA.

“Kuna vituo vya mafuta zaidi ya 3,000 nchini na katika vituo hivyo havizidi 600, ambavyo vimesajiliwa na NEMC na kupata EIA sasa kwa nchi nzima unapoongeza vituo vya mafuta bila kufuata sheria ni hatari sana,”alisema Dk. Gwamaka

Ameongeza kuwa kanuni zinataka umbali wa kituo kimoja cha mafuta hadi kingine usipungue mita 200, ili kuepusha athari kubwa zinazoweza kutokea wakati dharula ya moto, lakini kutokana na dharau ya wenye vituo hawazingatii kanuni hiyo.

Amesema wenye vituo vya mafuta wengi wamekuwa wakijenga na kisha kwenda kutafuta vibali baada ya ujenzi na wamekuwa wakivitafuta, kwa njia za rushwa na magendo.

Dk. Gwamaka amesema raia wanaozunguka eneo kinapojengwa kituo cha mafuta wana haki ya kushirikishwa na kupewa elimu kuhusu namna wanavyoweza kujiokoa inapotokea dharura.

“Sheria inawataka wenye miradi kuwashirikisha wananchi wa eneo husika kabla ya ujenzi wa vituo, ili watoe maoni na mawazo yao. Hiyo ni haki yao ya kisheria, ambayo hawapewi na hawa watu, lakini wanapata madhara makubwa ya kiafya,” alisema.

Amesema lengo la kutaka wenye miradi hiyo kuwashirikisha wananchi na kupata kibali cha EIA kabla ya ujenzi ni kujua usalama wa kiafya wa wananchi wanaozunguka maeneo ya mradi huo.